WAKAZI WA KAPENGURIA WAHIMIZWA KUTUMA MAOMBI YA FEDHA ZA BASARI KUTOKA HAZINA YA CDF.

Wakazi wa eneo bunge la Kapenguria katika kaunti ya Pokot Magharibi wamehakikishiwa kwamba shughuli ya utoaji wa fedha za basari kutoka kwa hazina ya CDF itatekelezwa kwa uwazi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari meneja wa hazina hiyo katika afisi ya mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, Paul Lolem alisema katika juhudi za kuhakikisha hilo, kila kata ndogo itakuwa na kamati mbili za kupiga msasa mchakato mzima wa utoaji fedha hizo.

Lolem alisema afisi hiyo imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuzuia kutokea lawama na propaganda ambazo zimekuwepo awali kuhusiana na jinsi shughuli nzima ya utoaji wa fedha hizo imekuwa ikiendeshwa.

“Tunawahakikishia wakazi kwamba tutazingatia uwazi mkubwa katika utoaji wa basari ya hazina ya CDF eneo bunge la Kapenguria. Tutabuni kamati mbili katika kila kata ndogo itakayopiga msasa mchakato mzima ili tuzuie lalama ambazo zimekuwepo awali kuhusu fedha hizo.” Alisema Lolem.

Mwenyekiti wa hazina hiyo Andrew Kodokwang alisema kipindi cha kutuma maombi kwa ajili ya fedha hizo kinaendelea hadi tarehe 27 mwezi huu, akiwataka wakazi kutumia kipindi hiki kutuma maombi.

Alisisitiza kwamba ni wakazi wa eneo bunge la Kapenguria pakee wanaoruhusiwa kutuma maombi hayo.

“Nawaomba wakazi wa eneo bunge la Kapenguria kutumia kipindi hiki kutuma maombi ya kupokea basari ya mbunge wa Kapenguria. Fomu za kutuma maombi zinapatikana katika mitandao, na pia tutazituma katika afisi za wasimamizi wa wadi pamoja na afisi za chifu.” Alisema Kodokwang.