KACHAPIN AAHIDI KUIMARISHA SHUGHULI YA UCHIMBAJI DHAHABU ROMUS.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameahidi kwamba serikali yake itahakikisha wakazi wa eneo la Romus Pokot kaskazini wananufaika na shughuli ya uchimbaji dhahabu ikiwa ndio shughuli ambayo wakazi hao wanategemea kujiendeleza kimaisha.
Akizungumza alipozuru eneo hilo, gavana Kachapin alisema kwamba serikali yake itawekeza pakubwa katika shughuli hiyo kwa kuandaa mazingira bora kwa wanaoiendeleza, ili kuhakikisha kwamba wengi wa wakazi wanapata ajira kupitia uchimbaji wa dhahabu.
Wakati uo huo Kachapin alisema kama gavana wa kaunti hiyo ni jukumu lake kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wanaendeleza shughuli zao kwa mazingira salama, hasa ikizingatiwa kumekuwa kukishuhudiwa uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa wahalifu wanaomainika kutoka kaunti jirani.
“Tunavyosema kaunti hii ina raslimali nyingi na hapa watu wengi wanajihusisha na uchimbaji wa dhahabu. Nawahakikishia wakazi wa eneo hili kwamba serikali yangu itahakikisha wachimbaji wa dhahabu wanapata mazingira bora ya kufanyia shughuli zao ili waweze kunufaika na shughuli hii.” alisema Kachapin.
Wakazi wa eneo hilo walipongeza ujio wa gavana wakielezea imani kwamba changamoto za kiusalama ambazo wamekumbana nazo kwa miaka mingi zitashughulikiwa, pamoja na kuhakikisha pia wananufaika na miradi ya maendeleo ikizingatiwa walisahaulika kwa miaka mingi.
“Kwa kipindi kirefu sisi hapa Romus tumekuwa tukikabiliwa na tatizo la usalama. Tumetelekezwa kwa miaka mingi sasa hasa kimendeleo, lakini sasa kwa vile gavana Kachapin yuko hapa tuna imani kwamba hali itakuwa salama.” Walisema.