WAAKILISHI WADI POKOT MAGHARIBI WASHIKILIA MSIMAMO WAO WA KUSITISHWA MARA MOJA KOMBE LA MURKOMEN.

Waakilishi wadi katika kaunti ya Pokot magharibi wamesisitiza msimamo wao kwamba kombe la murkomen ambalo linaandaliwa kwa ajili ya kuhimiza amani katika kaunti za bonde la kerio linafaa kusitishwa mara moja hadi patakaposhuhudiwa usalama katika kaunti hizi.

Wakizungumza siku moja tu baada ya gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin kusema kwamba kombe hilo litaendelea jinsi ambavyo iliratibiwa, viongozi hao walisema kombe hilo limefeli kuafikia malengo hasa ikizingatiwa linaandaliwa eneo ambako kunashuhudiwa amani na utulivu.

“Sisi kama wabunge katika bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi tunashikilia msimamo wetu kwamba kipute hiki cha Murkomen Cup kinafaa kusitishwa mara moja hadi pale tutakapoona usalama umeimarika bonde la kerio.” Walisema.

Aidha wabunge hao wa bunge la kaunti ya Pokot magharibi walipuuzilia mbali taarifa kwamba kaunti hiyo imepewa maafisa 205 wa akiba NPR kusaidia katika kuimarisha usalama maeneo ya mipakani, wakishikilia kuwa huo ni uvumi tu kwani hamna taarifa rasmi ya hatua hiyo kuchukuliwa kutoka wizara ya maswala ya ndani ya nchi.

“Kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba tumepewa maafisa wa NPR 205. Hizi bado ni fununu tu za mitandao. Sisi hatujapata taarifa rasmi kutoka kwa wizara ya usalama kwamba kaunti hii imepokezwa maafisa hao.” Walisema.

Viongozi hao waliendelea kulalamikia kile walidai serikali kushughulikia swala zima la utovu wa usalama katika kaunti za bonde la kerio kwa kuibagua kaunti hiyo, wakitaka silaha zilizokabidhiwa maafisa wa NPR katika kaunti za Turkana na Elgeyo marakwet kutwaliwa.

“Jamii ya pokot imetengwa pakubwa katika shughuli hii ya kuhakikisha usalama mipakani pa kaunti za kerio. Sasa tunasema kwamba iwapo serikali haitatusikiliza, basi watwae silaha ambazo zimekabidhiwa maafisa wa NPR katika kaunti jirani ili tuwe sawa.” Walisema.