SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA ZOEZI LA KUWAPA MIFUGO DAWA YA MINYOO.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia wizara ya kilimo na mifugo kwa ushirikiano na shirika la PSF Germany imeendeleza shughuli ya kuwapa mifugo dawa ya minyoo katika juhudi za kuimarisha mapato ya wafugaji.

Maafisa wa shirika hilo waliendeleza shughuli hiyo eneo la Chamage katika kata ya Miskwony alhamisi, chifu wa eneo hilo Reuben Chemoringot akitaja shughuli hiyo kuwa yenye umuhimu mkubwa zaidi ikizingatiwa wafugaji wamekuwa wakipata hasara kufuatia magonjwa ya minyoo ambayo yamekuwa yakiwahangaisha.

“Kabla ya chanjo ambayo tumeipata leo mifugo wetu wamekuwa wakiathirika pakubwa. Hata wakulima wakienda kujinunulia hawajui maelezo ya jinsi ya kuwapa mifugo dawa hizo. Lakini sasa vile maafisa hawa wamekuja, tunaamini kwamba mifugo wetu watabadilika kiafya.” Alisema Chemorigot.

Hata hivyo Chemoringot alilalamikia ukosefu wa maafisa wa mifugo waliohitimu eneo hilo, hali inayowapa changamoto ya kuafikia huduma muhimu kwa ajili ya mifugo wao huku pia wakipata ugumu wa kufikia afisi za serikali kupata huduma hizo kutokana na umbali.

“Hatuna maafisa wa mifugo ambao wamehitimu huku, na pia kufikia afisi za serikali inakuwa vigumu kwa sababu zipo mbali sana kutoka mahali tulipo. Kwa hivyo tunaomba wafadhili kujitokeza kwa wingi na kuja eneo hili ili nasi tunufaike na huduma kama hizi.” Alisema.

Wafugaji eneo hilo wakiongozwa na Paul Torong’uria wamepongeza hatua ya kuwapa mifugo wao dawa ya minyoo wakisema kwamba itaimarisha afya yao na hivyo kuwapelekea mazao ya kuridhisha.

Nashukuru sana maafisa hawa ambao wamekuja kuwapa mifugo wetu dawa ya minyoo. Itawasaidia sana  wanyama wetu wapate afya bora na kuimarika mazao yanayotokana na mifugo.” Walisema wafugaji.