WALIMU POKOT MAGHARIBI WAPONGEZWA KWA MATOKEO BORA YA KCPE.
Katibu mkuu wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la Pokot magharibi Martine Sembelo amewashukuru walimu na wazazi kwa kushirikiana na kuhakikisha kwamba wanafunzi katika kaunti hiyo wanafanya vyema katika mitihani ya kitaifa kwa darasa la nane KCPE.
Sembelo alisema kwamba licha ya changamoto mbali mbali ambazo zimeshuhudiwa, walimu walifanya juhudi kuhakikisha kwamba kaunti hiyo inasajili matokeo ya kuridhisha katika mitihani hiyo.
“Nawashukuru walimu na wadau wote wa sekta ya elimu katika kaunti hii kwa juhudi ambazo walitia licha ya changamoto mbali mbali kuhakikisha kwamba kaunti hii inasajili matokeo bora katika mtihani wa KCPE.” Alisema Sembelo.
Hata hivyo Sembelo aliwahimiza wazazi wa wanafunzi ambao huenda hawakusajili matokeo bora kulingana na matarajio yao, kutowakaripia watoto wao na badala yake kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo ikizingatiwa sasa kila mwanafunzi atapata nafasi katika shule ya upili licha ya matokeo.
“Ninachowahimiza wazazi ambao huenda watoto wao hawakufanya vyema katika mtihani huo jinsi walivyotarajia kwamba tusiwakaripie watoto hawa. Tukubali matokeo yao na kuendelea kuwaunga mkono katika elimu ya shule ya upili ikizingatiwa kila mwanafunzi atapata nafasi ya kuendelea.” Alisema.
Wakati uo huo Sembelo aliwahimiza wazazi kuwa karibu na wanao wakati huu ambapo wapo nyumbani kwa likizo, na pia kutumia wakati huu kuandaa karo kwa ajili ya masomo ya wanao shule zitakapofunguliwa mwakani.
“Kwa sababu sasa matokeo yametangazwa, ni vyema kwa wazazi kujiandaa kwa ajili ya karo. Tusijihusishe na sherehe nyingi hadi tumalize pesa na kisha tuanze kuhangaika shule zitakapofunguliwa. Pia wazazi tuwe karibu na watoto wetu na kuwapa mwelekeo mwema wakati huu ambapo wapo nyumbani.” Alisema.