ST. MARYS ASSUMPTION NA KAPENGURIA TOWN VIEW ZANG’ARA KATIKA MTIHANI WA KCPE POKOT MAGHARIBI.

Shule mbali mbali kaunti ya Pokot magharibi zimeendelea kusherehekea matokeo bora katika mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE ambayo yalitangazwa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu ikizingatiwa ndio mtihani wa mwisho katika mtaala wa elimu wa 8.4.4.

Miongoni mwa shule ambazo zilifanya vyema hadi kufikia sasa katika kaunti ya Pokot magharibi kulingana na matokeo haya ni St. marys Assumption ambapo mwanafunzi wa kwanza Sylvia Cherop alipata alama 419.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Gilbert Nyongesa alisema kwamba japo walitarajia zaidi ya hayo, matokeo ya shule hiyo yaliimarika mwaka huu ikilinganishwa na ya mwaka jana.

Alisema kwamba wamefurahia matokeo hayo licha ya changamoto nyingi ambazo walikumbana nazo, huku akiwapongeza wadau ikiwemo walimu na wazazi kwa ushirikiano mwema ambao alisema kwamba ulichangia matokeo hayo mema.

“Hadi kufikia sasa mwanafunzi wa kwanza katika shule hii amepata alama 419. Japo tulikuwa tunatarajia zaidi ya hayo, tunashukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu matokeo ya mwaka huu yameimarika ikilinganishwa na ya mwaka jana.” Alisema Nyongesa.

Katika shule ya kapenguria town view mwanafunzi wa kwanza Ritanyeng Subira alipata alama 413, akifuatiwa na Sharon Kizito kwa alama 412.

Katika shule ya Jerusalem academy mwanafunzi wa kwanza alipata alama 403, wa pili akipata 397, huku mwanafunzi wa kwanza katika shule ya msingi ya St. Michael akipata alama 405, wa pili akipata 404.

Aidha shule ya msingi ya Moorland academy eneo la Tapach ilisajili alama ya jumla ya 343 huku mwanafunzi wa kwanza akipata alama 410.