POLISI WA UGANDA WASUTWA KWA KUHATARISHA USALAMA WA WAKAZI WA KANYERUS POKOT MAGHARIBI.

Wakazi wa Kijiji cha Nasitit eneo la Kanyerus eneo bunge la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kudorora kwa hali ya usalama eneo hilo la mpakani pa kaunti hiyo na taifa jirani la Uganda.

Wakiongozwa na Benjamin Korir wakazi hao walielezea wasiwasi kuhusu mazoezi ambayo yanafanywa na maafisa wa polisi wa taifa jirani la Uganda, ambayo walidai kwamba risasi zinazotunika katika mazoezi hayo zinaelekezwa katika kijiji hicho cha Nasitit.

Wakazi hao sasa wametoa wito kwa viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi kuandaa kikao na wenzao kutoka Uganda kuhusiana na swala hilo wanalosema kwamba ni hatari kwa usalama wao.

“Kuna polisi wa kutoka Uganda ambao wanafanya mazoezi ya zana zao za kivita, ila hawajali sehemu ambazo wanaelekeza risasi ambazo zinatumika katika mazoezi haya. Mara kwa mara eneo hili limekuwa likilengwa na vifaa hivyo na sasa tuna wasi wasi na usalama wetu kama wakazi wa Nasitit.” Walisema.

Hata hivyo naibu kamishina eneo la Kacheliba Kenneth Kiprop aliwahakikishia wakazi hao kwamba wamezungumza na wakuu wa maafisa hao kuhusu kubadili eneo la kufanyia mazoezi ili kuzuia taharuki wanayosababisha miongoni mwa wakazi.

“Nitawaomba tu wakazi wa eneo hili kutokuwa na wasiwasi kwani tayari tumeandaa mazungumzo na viongozi katika idara ya usalama katika taifa jirani la Uganda, na wametuhakikishia kwamba hali hiyo haitatokea tena.” Alisema Kiprop.