WAFUGAJI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTOKOMEZA UGONJWA WA MIGUU NA MIDOMO.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia wizara ya kilimo imekeriri kujitolea kuhakikisha kwamba inamaliza ugonjwa wa mifugo wa miguu na midomo, ikitoa wito kwa wafugaji kushirikiana nayo katika juhudi za kukabili ugonjwa huu.
Waziri wa kilimo na mifugo kaunti hiyo Wilfred Longronyang aidha aliendelea kusisitiza haja ya wakulima kutii agizo la kusitishwa masoko ya mifugo kama njia moja ya kukabili kuenea kwa ugonjwa huu.
Longronyang alisema kwamba kama serikali walilazimika kusitisha masoko hayo ili kuzuia hali ambapo mifugo kutoka maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo watatangamana na kupelekea kuenea zaidi ugonjwa huo hali ambayo itafanya vigumu kukabiliana nao.
“Kama serikali tunawahakikishia wafugaji katika kaunti hii kwamba tutahakikisha ugonjwa wa miguu na midomo unatokomezwa. Kile ambacho ningependa kuwaomba wafugaji ni kwamba waendelee kutii agizo la kusitisha masoko ya mifugo ili tusaidie katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu. Hili ni agizo la muda tu na shughuli za kawaida zitarejelewa.” Alisema Longronyang.
Wakati uo huo Longronyang aliwataka wachuuzi pia kutofikiria tu jinsi ya kutengeneza pesa kwa kuendeleza biashara ya kununua na kuuza mifugo, bali pia kuwazia kuhusu hali ya wakulima pamoja na afya ya wananchi, na kushirikiana na serikali ili kumaliza ugonjwa huu.
“Wachuuzi pia wasiwe watu wenye tamaa, wakifikiria tu jinsi ya kutengeneza pesa bila ya kuwazia hali ya wafugaji na pia afya ya wananchi. Wakati wanapoendeleza biashara hii ya kuuza mifugo kutoka eneo moja hadi lingine wanasambaza ugonjwa huu. Naomba sote tushirikiane ili tumalize ugonjwa huu.” Alisema.