WAHUDUMU WA AFYA CHPs POKOT MAGHARIBI WAPOKEZWA VIFAA VYA KURAHISISHA SHUGHULI ZAO MASHINANI.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza serikali kuu kupitia wizara ya afya kwa kuwapokeza wahudumu wa afya wa nyanjani CHPs vifaa ambavyo watatumia katika kutekeleza shughuli zao hasa maeneo ya mashinani.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo kutoka kwa waziri wa afya Suzan Nakhumicha afisini mwake, gavana Kachapin alisema kwamba vifaa hivyo ni muhimu sana kwani vitawarahisishia wahudumu hao kazi yao ikilinganishwa na jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya awali.
“Lengo la waziri kuja hapa ni kuwapokeza hawa wahudumu simu za kidijitali ili kurahisisha kazi yao, na nimefurahi sana kumkaribisha waziri hapa kwa sababu hawa CHPs wanafanya kazi nzuri.” Alisema Kachapin.
Kachapin alisema serikali yake inaunga mkono kikamilifu mikakati ambayo serikali ya kitaifa inaweka katika kuhakikisha kwamba idara ya afya inaimarika, hasa ikizingatiwa kwamba kaunti hiyo ilisalia nyuma kwa muda kutokana na swala la afya.
“Mimi na serikali yangu tunaunga kikamilifu mikakati ambayo serikali ya kitaifa inaweka kuimarisha sekta ya afya, kwa sababu inaenda kuhakikisha kwamba huduma zinaimarika ikizingatiwa kaunti imesalia nyuma kwa muda mrefu.” Alisema.
Kwa upande wake waziri Nakhumicha alisema kwamba ameikabidhi kaunti hiyo jumla ya simu 2,423 za kidijitali ili kuhakikisha kwamba kila mhudumu wa afya wa nyanjani CHP anapokea simu hiyo itakayowasaidia kuhifadhi data zao kwa njia ya dijitali.
“Katika kaunti hii ya Pokot magharibi tuna wahudumu wa afya wa nyanjani 2,423. Tumewapa mafunzo na sasa tumewakabidhi kila mmoja simu ya kidijitali, kwa sababu tunataka kazi yao iwe rahisi. Wakiingia maeneo ya mashinani watatumia simu hizi kuhifadhi data kuhusu nyumba wanazotembelea kutoa huduma.” Alisema Nakhumicha.