MENGICH APONGEZA HATUA YA DCI KUWAHOJI BAADHI YA VIONGOZI WA TURKANA KUHUSIANA NA USALAMA.

Mwakilishi wadi ya seker kaunti ya Pokot magharibi Jane Mengich amepongeza hatua ya idara ya upelelezi DCI kuwahoji  viongozi wawili katika kaunti ya Turkana kuhusiana na utovu wa usalama ambao unashuhudiwa mipakani pa kaunti za bonde la kerio.

Mengich alidai kwamba viongozi hao wamekuwa wakijihusisha na matamshi ya kiholela hali anayodai ni tishio kwa juhudi ambazo zinaendelezwa za kuafikiwa usalama katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa.

Jumanne wiki hii mwakilishi kina mama katika kaunti hiyo ya Turkana Cecilia Ngitit na mbunge wa Turkana mashariki Nicholas Ngikor walifika katika afisi za idara hiyo ambapo walihojiwa kuhusiana na hali ya usalama inayoshuhudiwa maeneo haya.

“Nafurahia sana hatua ya mwakilishi kina mama wa kaunti ya Turkana na mbunge wa Turkana ya mashariki kuandikisha taarifa na idara ya DCI kuhusiana na matamshi ambayo wamekuwa wakitoa kwenye mikutano ya hadhara. Nimekuwa nikisema kwamba viongozi hawa wanatoa matamshi ambayo ni hatari kwa usalama wa eneo hili.” Alisema Mengich.

Hata hivyo Mengich alitaka gavana wa kaunti hiyo Jeremiah Lomurkai pia kuagizwa kufika katika afisi za DCI kuandikisha taarifa kuhusiana na matamshi ambayo amedai kwamba ni ya uchochezi na ambayo amekuwa akiyatoa gavana huyo katika mikutano ya umma.

“Kuna mtu mmoja ambaye amesalia kuitwa na DCI, na huyu ni gavana wa kaunti hiyo ya Turkana Jeremiah Lomurkai. Yeye pia amekuwa akitoa matamshi ya kiholela kwenye mikutano ya umma na anafaa kuchunguzwa.” Alisema.