MAHAKAMA YA KAPENGURIA YAZINDUA MWEZI WA KUSHUGHULIKIA KESI ZA WATOTO.

Mahakama ya kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi imezindua rasmi mwezi wa kushughulikia kesi zinazowahusu watoto kwa haraka katika mwendelezo wa shughuli hiyo ambayo hutengewa mwezi Novemba kila mwaka.

Jaji wa mahakama hiyo Justice Anthony Mrima alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo ambao wana kesi ambazo zinahusu watoto kutumia fursa hii kuwasiliana na idara husika ili kesi hizo zishughulikiwe, akisema kwamba wanalenga kukamilisha kesi hizi ifikiapo mwisho wa mwezi huu.

“Kila mwaka Mahakama huwa imetenga mwezi Novemba kuwa mwaka wa kushughulikia kesi zinazohusu watoto. Tunatoa wito kwa wakazi ambao wana kesi za aina hiyo kuwasiliana na idara husika ili kesi hizo ziweze kushughulikiwa. Tunataraji kwamba kufikia mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumeshughulikia kesi zote.” Alisema Mrima.

Aidha jaji Mrima alisema kwamba kesi nyingi zinazohusu watoto chini ya umri wa miaka 18 ambazo zinawasilishwa katika mahakama hiyo zinahusu ubakaji pamoja na maswala yanayohusiana na urithi, hasa katika hali ambapo wazazi wa mhusika wameaga dunia.

“Kesi zinazohusiana na watoto ambazo tunapokea kwa wingi katika mahakama hii ni zile zinazohusu ubakaji wa watoto chini ya umri wa miaka 18. Pia kuna kesi ambazo zinahusu uridhi katika tukio ambapo wazazi wameaga dunia japo hizi si nyingi sana.” Alisema.

Wakati uo huo Mrima alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kukumbatia huduma za mahakama akisema kwamba idara ya mahakama imefanyiwa mageuzi makubwa tangu kuanza kutekelezwa katiba mpya nchini na kuboresha huduma zake.

“Tangu tulipopata katiba mpya mahakama imepitia mageuzi makubwa sana. Si ile mahakama ambayo tulikuwa tukifahamu katika miaka ya awali ambapo watu walikuwa wakiiogopa. Kwa sasa koti ina ubinadam na tujaribu sana jinsi tuwezavyo ili kuwahudumia watu kwa yale mahitaji waliyo nayo.” Alisema.