IDARA YA MIPANGO NA MAENDELEO YAENDELEZA VIKAO VYA KUKUSANYA MAONI KUHUSU BAJETI.

Maafisa kutoka idara ya mipango na maendeleo katika serikali kuu wamezuru kaunti ya Pokot magharibi kupokea maoni ya wananchi katika vikao ambavyo inaendelezwa katika ngazi za kaunti kwa lengo la kuhakikisha kwamba bajeti inayoandaliwa inawiana na mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na wanahabari baada ya shughuli hiyo afisa katika idara hiyo Jacob Mulwa alielezea umuhimu wa kuwahusisha wananchi katika maandalizi ya bajeti akisema kwamba inasaidia kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaafikia mahitaji ya mwananchi.

Aidha Mulwa alisema kupitia shughuli ya kukusanya maoni, wananchi wanapata kufahamu changamoto ambazo zinalikumba taifa, akiwahimiza kujitokeza na kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuwasilisha maoni yao panapoandaliwa vikao kama hivi.

“Tunaheshimu katiba yetu na katiba inampa mwananchi nguvu ya kuamua anachotaka kufanyiwa kupitia vikao vya maoni. Na nikao hivi vinalenga kuhakikisha kwamba maoni ya mwananchi yanawianishwa na bajeti. Pia vikao hivi vitasaidia wananchi kufahamu changamoto ambazo zinakabili taifa letu.” Alisema Mulwa.

Mulwa alisema kwamba idara hiyo inaangazia kwanza miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa kabla ya kutoa mipangilio ya kufadhili miradi mipya kutokana na uchache wa raslimali.

“Tuna raslimali kidogo sana na ndio maana tunatoa kipau mbele kwa miradi ambayo inaendelea kabla ya kuanzishwa mingine mipya.” Alisema.