KACHAPIN: MAONYESHO YA KILIMO YATATUMIKA KUBADILI SURA YA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI MACHONI PA ULIMWENGU.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesema maonyesho ya kilimo ambayo yanatarajiwa kuandaliwa katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Kishaunet kaunti hiyo yatatumika kudhihirishia ulimwengu kwamba kaunti hiyo ni salama kinyume na ambavyo imekuwa ikidhaniwa.
Akizungumza wakati akikagua maandalizi ya maonyesho hayo ya siku tatu ambayo yataanza tarehe 8 hadi 11 mwezi Novemba mwaka huu, Kachapin alisema kwamba maonyesho hayo yatatumika kudhihirisha uwezo wa kaunti hiyo si tu kuhusu maswala ya kilimo bali pia utamaduni aliosema kwamba una utajiri mkubwa.
Kachapin alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo pamoja na wanachi kutoka maeneo mbali mbali ya taifa hili kujitokeza kwa wingi na kuhudhuria maonyesho hayo aliyotaja kwamba yatakuwa ya manufaa makubwa katika shughuli za kilimo hasa kuhusu mbinu za kisasa za kilimo katika ulimwengu unaobadilika kiteknolojia.
“Nawakaribisha wakazi wote wa kaunti hii na hata kaunti zingine katika maonyesho ya kilimo ambayo yataandaliwa kwemnye uwanja wa Kishaunet, ambayo pia yatatumika kuonyesha utamaduni wetu ambao una utajiri mkubwa. Tunalenga pia kutumia maonyesho haya kuonyesha ulimwengu kwamba Pokot magharibi ni kaunti ambayo ni salama kinyume na jinsi imekuwa ikiaminika.” Alisema Kachapin.
Wakati uo huo gavana Kachapin alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa kaunti hiyo kujitenga na siasa za mapema na badala yake kushirikiana katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapokea maendeleo inavyopasa, na pia kumpa muda wa kuhakikisha kwamba anatimiza mipango yake kwa wakazi.
“Sasa si wakati wa kuanza kulumbana kisiasa. Sasa ni wakati ambapo kila kiongozi ambaye alichaguliwa anapasa kuhakikisha kwamba anahudumia wanachi na kuwahakikishia maendeleo. Mimi kama gavana nina mipango ambayo nimeweka na nataka kutumia muda huu kuhakikisha kwamba natekeleza mipango hiyo kwa wananchi wala si kujihusisha na siasa za kila mara.” Alisema.