SHINIKIZO ZA KUBAINISHWA MIPAKA YA KAUNTI ZA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA ZAENDELEA KUTOLEWA.

Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kutoa wito kwa serikali kuendesha zoezi la kubaini mipaka baina ya kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana.

Wa hivi punde kutoa wito huo ni mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alisema kwamba mizozo ambayo imekuwepo baina ya viongozi wa kaunti hizi mbili kuhusu mipaka itapata tu suluhu kupitia kuwekwa wazi mipaka hiyo.

 “Jinsi wenzetu wanasema kwamba wanataka mipaka ijulikane, mimi nakubaliana nao. Serikali ije itueleze mpaka wa kaunti ya Pokot magharibi na Turkana ili tujue. Na baada ya kujulikana tuone sasa watu wanaishi upande gani wa huu mpaka.” Alisema Lochakapong.

Lochakapong alitoa wito kwa viongozi kuwa makini na matamshi yao wanaposhinikiza swala la kubainisha mipaka hiyo na kutoingiza jamii katika shinikizo hizo hali aliyosema huenda ikachochea tofauti baina ya jamii za kaunti hizi.

“Swala la mipaka baina ya kaunti hizi mbili halifai kuingizwa jamii. Watu wako huru kuishi upande wowote, iwe ni Turkana au Pokot magharibi. Tukianza kusema kwamba wapokot au waturkana wanafaa kuishi wapi basi tutakuwa tunachochea uhasama baina ya jamii hizi mbili.” Alisema.

Wito wake Lochakapong unajiri siku moja tu baada ya mwakilishi wadi ya Seker Jane Mengich kumsuta gavana wa kaunti ya Turkana Jeremiah Lomurkai kwa kile alidai kutaja maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi kuwa ardhi ya Turkana.