UFUGAJI WA KUHAMAHAMA WATAJWA KUWA KIKWAZO KWA SHUGHULI ZA ELIMU MAENEO KAME.

Wadau katika sekta ya elimu maeneo yanayokumbwa na ukame katika kaunti ya Pokot magharibi wametoa wito kwa serikali kuweka mikakati itakayohakikisha kwamba wazazi maeneo hayo hawahami ili kutafuta lishe kwa ajili ya mifugo yao.

Wakiongozwa na Evanjeline Wekesa, mwalimu katika shule ya msingi ya Mbaru eneo la Kiwawa, wadau hao walisema kwamba hatua ya wazazi kuhamahama katika juhudi za kuwatafutia lishe mifugo inaathiri pakubwa elimu ya watoto hasa wa kike.

Aidha, wadau hao walitoa wito kwa serikali kuanzisha miradi ya kilimo itakayowasaidia wakazi wa maeneo hayo kujikimu kimaisha, ili kuzuia hali ambapo wengi wa watoto hutumwa kutafuta dhahabu hali ambayo inahatarisha maisha ya watoto pamoja na kuathiri masomo.

“Natoa wito kwa serikali kuanzisha miradi ambayo itawawezesha wazazi kukimu mahitaji yao na mifugo wao kwa sababu hii hali ya wazazi kuhamahama ili kutafutia mifugo lishe imeathiri sana masomo ya watoto maeneo haya.” Alisema Evanjeline.

Kauli yake ilisisitizwa na Margaret Munari mwalimu katika shule ya msingi ya chelopoy ambaye alisema  ukame umepelekea umasikini katika jamii nyingi maeneo hayo hali ambayo inawafanya wengi wa wazazi kuwaoza mapema wanao ili kupata mali itakayowawezesha kujikimu kimaisha, na hivyo kuwakatizia ndoto zao maishani.

“Wengi wa wazazi eneo hili hawajihusishi na kilimo kwa sababu ya ukame. Sasa wengi wao wanaishi katika hali ya umasikini, swala ambalo linachangia pakubwa kwa wengi wao kuamua kuwaoza mapema wanao kwa lengo la kupata mali.” Alisema Munari.