MASHAMBULIZI YAENDELEA KUSHUHUDIWA TURKWEL LICHA YA IDARA YA USALAMA KUWAHAKIKISHIA WAKAZI USALAMA.
Watu wawili wakazi wa eneo la Turkwel katika kaunti ya Pokot magharibi wanauguza majeraha ya risasi katika hospitali ya Kapenguria baada kuvamiwa na watu wanaokisiwa kutoka kaunti jirani.
Tukio hili linajiri siku moja tu baada ya maafisa wa idara ya usalama wakiongozwa na kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Peter Katam kufanya kikao na wakazi wa eneo hilo, kuangazia hali ya usalama ambapo aliwahakikishia kwamba watahakikisha usalama unadumishwa eneo hilo.
Wakazi wa eneo hilo walilalamikia uvamizi huo wa mara kwa mara ambao walisema umewalazimu kukesha nje nyakati za usiku kwa hofu ya kuvamiwa na wahalifu, wakilaumu serikali kwa kutochukua hatua za kuhakikisha kwamba swala hilo linashughulikiwa upesi.
“Sisi huku tumehangaishwa sana na wahalifu. Hatuna mahali pa kulala usiku. Tunalazimika kukesha msituni kwa sababu hatuwezi kuelekea kwa nyumba zetu.” Walisema.
Aidha wakazi hao waliwalaumu maafisa wa usalama ambao wanaendesha oparesheni ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria katika kaunti za bonde la kerio, kwa kutekeleza oparesheni hiyo kwa mapendeleo.
Walidai kwamba maafisa hao wametwaa bunduki zote ambazo zilikuwa zikimilikiwa na wakazi wa kaunti hiyo huku wakazi wa kaunti jirani wakiendelea kumiliki bunduki hizo ambazo wanadai kwamba wanazitumia kutekeleza uvamizi.
“Hawa polisi wanaoendeleza oparesheni ya kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria wanafanya kwa mapendeleo. Wamepokonya wakazi wote wa Pokot huku wakiachia majirani zetu silaha ambazo wahalifu wanatumia kutuhangaisha.” Walisema.