WAKAZI WA JAMII YA POKOT ENEO LA TIATI WASHINIKIZA KUBUNIWA KAUNTI YAO.

Viongozi kutoka jamii ya Pokot kaunti ya Baringo wameunga mkono pendekezo la kuongezwa idadi ya kaunti nchini wakidai kwamba hali hiyo itapelekea huduma sawa kwa jamii zote.

Wakizungmza eneo la Tangulbei eneo bunge la Tiati, viongozi hao wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Tirioko Sammy Lokales walidai kwamba jamii ya Pokot imetengwa pakubwa katika uongozi wa kaunti ya Baringo na sasa ni wakati wanapasa kujitawala katika kaunti yao wenyewe.

Walitaka eneo la Tiati kufanywa kaunti na kuitwa pokot mashariki ili kuhakikisha kwamba raslimali zinawafikia wakazi wa eneo hilo.

“Sisi tunataka kaunti ya Tiati, pokot mashariki iongezwe ili watu wa jamii ya Pokot waweze kujitawala kwa sababu tumetengwa sana katika serikali ya kaunti hii ya Baringo. Tunataka pia raslimali ziweze kuwa karibu nasi.” Alisema Lokales.

Viongozi hao walisema kwamba wameachwa nyuma kwa miaka mingi hasa katika tawala zilizotangulia, na sasa hawangependa hali hiyo kuendelea katika utawala wa rais William Ruto ambaye wanasema kwamba ameonyesha nia ya kuhakikisha maeneo yote nchini yanafikiwa na huduma za serikali.

“Tumeachwa nyuma kwa miaka mingi sana hasa na serikali zilizotangulia. Tumeona mwanga kidogo tu wakati wa utawala wa rais wa sasa William Ruto. Hatungependa kuendelea kuishi kama jamii ambayo imetengwa.” Alisema.