ZOEZI LA KUWASAJILI WAKULIMA POKOT MAGHARIBI LATARAJIWA HUKU WAKULIMA WAKITAKIWA KUJITOKEZA KATIKA ZOEZI HILO.

Waziri wa kilimo, mifugo, uvuvi na unyunyiziaji maji mashamba kaunti ya Pokot magharibi Wilfred Longronyang ametoa wito kwa wakulima kujitokeza ili kusajiliwa katika zoezi la usajili wa wakulima ambalo linatarajiwa kutekelezwa mwishoni mwa mwezi huu wa octoba.

Akizungumza na wakulima eneo la Murkwijit, Longronyang alisema kwamba zoezi hilo ni muhimu kwani linatoa fursa kwa wakulima kufahamu idadi ya mifugo au mimea wanaoyomiliki katika mashamba yao.

Alisema hali hii itafanya rahisi kwa serikali kufanikisha miradi ya maendeleo inayohusiana na kilimo maeneo mbali mbali kulingana na aina ya kilimo ambacho kinaendelezwa maeneo hayo.

“Kutakuwa na zoezi la kuwasajili wakulima katika kaunti hii mwishoni mwa mwezi octoba. Nawaomba wakulima wote kujitokeza na kusajiliwa katika zoezi hili ili ifahamike mifugo na mimea ambayo iko mashambani mwao na kufanya rahisi kwa serikali kutekeleza miradi ya kilimo.” Alisema Longronyang.

Aidha Longronyag aliwataka wakulima kuhakikisha kwamba wanajumuisha kila wanachomilika wakati wa usajili huo.

“Wakati wa usajili huo tutawataka wakulima kuhakikisha kwamba wanasajili mifugo wao wote ambao wanamiliki. Ni muhimu kufahamu idadi kamili ya mifugo wanayomiliki katika mashamba yao.” Alisema.

Wakati uo huo Longronyang alitumia fursa hiyo kuwaonya wakulima ambao wanafanyia biashara mbolea inayotolewa na serikali kwa bei nafuu kwa kuiuza kwa bei ya juu, huku akiwahimiza wakulima kuhakikisha mbolea iliyotolewa katika msimu uliopita inatumika kabla ya awamu nyingine kutolewa.

“Kuna baadhi ya wakulima ambao wanachukua mbolea inayotolewa na serikali kwa bei ya chini na kisha kuwauzia wenzao kwa bei ghali. Hii tabia hatutakubali hata kidogo. Hakikisha kwamba unatumia mbolea yote ambayo ilitolewa katika awamu ya kwanza kabla ya kupokea kwenye awamu inayotarajiwa.” Alisema.