SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA UTALII.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba inapata mapato kupitia utalii.
Akizungumza eneo la Keringet wakati wa kuadhimisha siku ya utalii duniani, waziri wa utalii, michezo, vijana na utamaduni katika kaunti hiyo Joshua Siwanyang alisema, serikali imewekeza pakubwa katika ujenzi wa hoteli kubwa ambazo zitatumika kuwapa sehemu za kula na kulala watalii wanaozuru kaunti hiyo ili kuhakikisha fedha zinazotumika kutafuta huduma hizo kwingine zinasalia kaunti hiyo.
“Tumewekeza sana katika ujenzi wa hoteli kubwa kubwa katika kaunti hii ili kuwapa sehemu ya kula na kulala watalii wanaozuru kaunti hii katika juhudi za kuhakikisha kwamba fedha zinazotumika kutafuta huduma hizo zinasalia hapa.” Alisema Siwanyang.
Aidha siwanyang aliwataka wakazi wa eneo la utalii la Keringet Swamp kutunza mazingira ili kuhifadhi ndege wanaopatikana eneo hilo ambao ndio hutumika kama kivutio kwa watalii,na ambao alisema kwamba ni wa aina ya kipekee wasiopatikani kwingine.
“Nahimiza jamii inayoishi eneo hili kutunza mazingira ili wale ndege wanaopatikana katika eneo hili wasije wakapotea kwa sababu kuna aina ya ndege ambao hawapatikani kwingine.” Alisema.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la msalaba mwekundu Mark John alipendekeza eneo hilo la kitalii kuzungushiwa ua ambao utahakikisha linahifadhiwa vyema hatua itakayowavutia watalii zaidi.
“Tuhakikishe kwamba eneo hili linazungushiwa ua na kuhakikisha kwamba linasalia salama ili kuwavutia watalii zaidi.” Alisema John.