KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI YAPOKEA SHEHENA YA VIFAA VYA MATIBABU.
Huduma za afya zinatarajiwa kuimarika kaunti ya Pokot magharibi baada wizara ya afya kaunti hiyo kupokea shehena ya kwanza ya vifaa vya matibabu vitakavyotumika na wahudumu wa afya maeneo ya mashinani.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo katika hospitali ya Kapenguria, afisa mkuu wa wizara ya afya katika kaunti hiyo Nelly Soprine alisema kwamba vifaa hivyo vitasaidia pakubwa katika kuimarisha afya ya wakazi hasa maeneo ya mashinani.
Aidha Soprine alisema vifaa hivyo ni hatua kubwa ya juhudi za kuafikia mpango wa afya kwa wote UHC.
“Tumepata shehena ambayo ina vifaa 486 vitakavyowawezesha wahudumu wa afya kuendeleza huduma za matibabu katika maeneo ya mashinani. Vifaa hivi vitasaidia pakubwa katika juhudi za kuafikia mpango wa afya bora kwa wote katika kaunti hii.” Alisema Soprine.
Naibu mkurugenzi wa afya ya umma Abel Koech alisema kwamba kupitia vifaa hivyo magonjwa mengi yataweza kuzuiwa kwani vitasaidia katika kutambua mapema magonjwa mbali mbali na kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba yanakabiliwa miongoni mwa jamii.
“Kupitia vifaa hivi tutakuwa katika nafasi bora ya kukabili magonjwa kwa sababu vitatusaidia sana kuyatambua magonjwa mapema na kuyakabili kabla ya kufikia viwango hatari.” Alisema Koech.
Vifaa hivyo vya matibabu vilizinduliwa rasmi na rais William Ruto jumatatu wiki hii.