JAMII YATAKIWA KUKUMBATIA MBINU ZA UPANGAJI UZAZI ILI KUKUZA KIZAZI CHENYE AFYA.
Ipo haja ya jamii kukumbatia mbinu za upangaji uzazi ili kukuza kizazi chenye afya hasa hali ya maisha inapoendelea kubadilika kila kuchao kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha.
Akizungumza eneo la Kabichbich kaunti ya Pokot magharibi wakati wa maadhimisho ya siku ya upangaji uzazi, afisa katika shirika la DSW Peris Chepeng’at alisema nyingi ya familia kaunti hiyo zimekosa kutimiza mahitaji ya familia zao kutokana na kutopangilia uzazi.
“Kulingana na takwimu, katika kaunti hii inakadiriwa kwamba mama mmoja ana takriban watoto saba. Kwa hivyo huo unakuwa ni mzigo kwa mzazi kwa sababu idadi hii ina maana kwamba huenda akakosa kutimiza mahitaji ya muhimu ya watoto, kama kiafya na hata kielimu.” Alisema Chepeng’at.
Afisa mkuu katika wizara ya afya kaunti hiyo Nelly Soprin alielezea umuhimu wa jamii kukumbatia mbinu za kupanga uzazi, akisema kwamba kina mama ambao wanakosa kutumia mbinu hizi wako katika hatari ya kudhoofika kiafya kauli yake ikisisitizwa na naibu chifu wa Mbayai eneo la Lelan Julius Mkeng’ole.
“Matatizo ya kutopanga uzazi ni kwamba afya ya mama hudhoofika kutokana na kupungua kinga mwilini. Na kutokana na kinga kuwa chini mama anaweza kupoteza ujauzito au hata kupoteza maisha mwenyewe.” Alisema Soprin.
Kwa upande wake Consolata Sire ambaye ni afisa katika wizara ya afya kaunti hiyo anayesimamia kitengo cha afya ya akina mama na watoto, alisema kuna hatua ambazo zimepigwa katika juhudi za kuhakikisha kwamba jamii inakumbatia mbinu hizi kufuatia uhamasisho ambao umekuwa ukitolewa.
“Tangu tuanze kutoa uhamasisho kwa wakazi wa kaunti hii kuhusu swala la upangaji uzazi, tumepiga hatua kwani sasa watu wetu wanaelewa kwamba kupanga uzazi kuna manufaa makubwa kwa familia ikilinganishwa na miaka ya awali.” Alisema Sire.