UMASIKINI MIONGONI MWA KINA MAMA WATAJWA KUWA CHANZO KIKUU CHA DHULUMA ZA KIJINSIA.

Umasikini na hali ya wanawake kuwategemea zaidi waume zao kwa mahitaji yao mengi hasa ya kimsingi ndio maswala ambayo yametajwa kuchangia zaidi visa vya ukeketaji na dhuluma za kijinsia miongoni mwa jamii katika kaunti ya Pokot magharibi.

Kulingana na mkurugenzi wa shirika la Centre for Indigenous Child Rights (CICR) Everlyne Prech, shirika hilo lililazimika kuendesha utafiti wa kubaini kinachosababisha kuendelea kushuhudiwa visa hivi licha ya mikakati ya kuvikabili, ikibainika kwamba wengi wa wanawake wanakabiliwa na hali kubwa ya umasikini hali inayowalazimu kuwategemea waume zao.

“Sisi kama shirika tulifanya utafiti ili kubaini ni kwa nini visa vya ukeketaji na dhuluma za jinsia vimeendelea kuripotiwa licha ya mikakati ambayo inawekwa kukabili visa hivi. Tuligundua kwamba hali ya umasikini miongoni mwa wanawake na kutegemea zaidi waume zao ndio vyanzo vikuu vya visa hivi.” Alisema Prech.

Prech alisema hali hii imewafanya wanawake kujisalimisha kupitiliza na kuwapelekea kukubali lolote wanalotaka waume zao, na hivyo kuwa vigumu kukabili visa hivi, hali ambayo imepelekea shirika hilo kuanzisha miradi mbali mbali ya kuwawezesha wanawake kama njia moja ya kuwafanya kujitegemea.

“Kutokana na hali kwamba kina mama hawana uwezo wa kifedha, wanategemea zaidi waume zao na kulazimika kujisalimisha kupitiliza. Hali hii inafanya kutokuwa na usemi mbele ya waume zao. Kama shirika, tulianza miradi mbali mbali ya kuwawezesha kina mama kifedha ambapo baada ya muda wengi wao sasa wanaweza kujitegemea.” Alisema.

Alisema kwamba kupitia mafunzo ambayo yanatolewa na shirika hilo, wengi wa watoto wa kike wameokolewa kutokana na tamaduni ya ukeketaji na hivyo kuwapa nafasi ya kuendeleza masomo yao ili kuafikia ndoto zao maishani.

“Tangu tulipoanza shughuli zetu kupitia mpango huu tumeweza kuokoa wasichana wengi kutokana na ukeketaji ambapo wengi wao wamesoma hadi kufika vyuo vikuu na hivi wanaweza kutimiza ndoto zao maishani.” Alisema.