MWANAMKE AWATEKETEZA WATOTO WA MKE MWENZA NA KUTOWEKA KAPCHOK, POKOT MAGHARIBI.

Polisi eneo la Kapchok kaunti ya Pokot magharibi wanamsaka mwanamke mmoja anayedaiwa kuwateketeza watoto watatu baada ya kuwafungia katika chumba ambacho kilikuwa kimeezekwa kwa nyasi katika kijiji cha Kalukuna wadi ya Kapchok.

Kulingana na wanakijiji, mshukiwa ni mwanamke ambaye ameolewa hivi karibuni akiwa mwanamke wa nne katika boma hilo, na alikuwa bado hajapata mtoto, hali iliyomfanya kuomba kukaa na watoto wa wake wenza.

“Huyu mama aliolewa hapa majuzi tu akiwa mke wa nne sasa na hakuwa na mtoto. Aliwaomba wake wenza kumpa watoto hawa ili angalau akae nao kwa sababu hakutaka kuwa peke yake wakati mmewe hayuko.” Walisema wanakijiji.

Mwanamke huyo alitekeleza unyama huo usiku wa kuamkia jumatatu wakati mmewe alikuwa kwa mke mwenza, japo haikubainika mara moja kilichompelekea kuchukua hatua hiyo ya kinyama kabla ya kutoweka.

“Baada ya mmewe kuondoka kwenda kwa mke wake mwingine, huyu mama aliamua kwafungia hawa watoto kwenye nyumba na kisha kuwasha hiyo nyumba ambayo ilikuwa imeezekwa kwa nyasi na kuwateketeza watoto na kisha akatoweka.” Walisema.

Maafisa wa polisi walifika kwenye eneo la tukio na kuchukua miili ya watoto hao wenye umri wa miaka minne, sita na saba mtawalia huku uchunguzi ukiendelea.