RAIS RUTO AENDELEA KUPOKEA SHUTUMA KWA ‘KUKIUKA’ AHADI ALIZOTOA KWA WAKENYA KUHUSU GHARAMA YA MAISHA.
Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameelezea kusikitishwa na kile walisema kwamba rais William Ruto kwenda kinyume na ahadi ya kupunguza gharama ya maisha aliyotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Wakiongozwa na Joseph Sarich, wakazi hao walitaja hatua ya kuongezwa bei ya mafuta kuwa inayolenga kuwakandamiza zaidi wananchi wa hali ya chini ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu kufuatia kupanda gharama ya maisha.
Sarich alisema matarajio ya wananchi yalikuwa juu mno kuhusiana na uongozi wa rais Ruto hasa baada yake kuikosoa mara kwa mara serikali iliyotangulia kwa kile alidai kuwanyanyasa wananchi, lakini sasa hali inayoshuhudiwa nchini ni tofauti sana na jinsi walivyotarajia.
“Wananchi wameumia sana chini ya serikali hii ya Kenya kwanza. Gharama ya maisha imepanda zaidi kufuatia kuongezwa kiholela bei za mafuta. Wakati rais akifanya kampeni, alituhadaa kwamba atashughulikia gharama ya juu ya maisha lakini sasa baada ya kupata uongozi lugha yake imebadilika kabisa.” Alisema Sarich.
Sarich alidai kwamba rais aliwahadaa wananchi kwa lengo la kupata kura ili aongoze taifa, ambapo kulingana naye katika kipindi cha mwaka mmoja ambao rais Ruto amekuwa mamlakani hamna ahadi ambayo ametimiza.
Alidai huenda rais analenga kuwahangaisha wakenya katika kipindi hiki ili kupunguza gharama ya maisha mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kuwavutia wakenya kumpigia tena kura.
“Hamna ukweli wowote kwa yale yote ambayo rais Ruto aliahidi. Mwaka mmoja ambao amekuwa uongozini hamna ahadi ambayo ametimiza, na najua kwamba anataka kuwahangaisha wananchi na gharama ya juu ya maisha kwa sasa ili uchaguzi mkuu ujao ukikaribia, atudanganye na kuteremesha gharama ya maisha kwa lengo la kupata kura za wananchi.” Alisema.