WAZAZI WALAUMIWA KWA KUKITHIRI MIMBA ZA MAPEMA MIONGONI MWA WANAFUNZI POKOT MAGHARIBI.

Katibu wa chama cha walimu nchini KNUT tawi la kaunti ya Pokot magharibi Martine Sembelo amewalaumu pakubwa wazazi kufuatia ongezeko la mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi kaunti hiyo.

Akizungumza afisini mwake mjini Kapenguria, Sembelo alisema kwamba wazazi wameacha jukumu lao la kuwashauri watoto wao dhidi ya kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi wakiwa wangali shuleni.

Aidha Sembelo aliwataka walimu kutoendeleza unyanyapaa dhidi ya wanafunzi wa kike ambao wanarejea shuleni baada ya kujifungua na badala yake kuwapa nafasi na mazingira bora ya kuendeza masomo yao.

“Kina mama wameacha jukumu lao la kuwashauri watoto wao wa kike, na ndio maana tunaona mimba za mapema zikiongezeka miongoni mwa wanafunzi. Tunawahimiza pia kina baba kuhakikisha kwamba wanaketi na watoto wao wa kiume na kuwakumbusha kwamba watachukuliwa hatua iwapo watapachika mwanafunzi mimba.” Alisema Sembelo.

Wakati uo huo Sembelo alitoa wito kwa idara za usalama kuzidisha doria maeneo ya mipakani ambako kunashuhudiwa utovu wa usalama unaosababishwa na wezi wa mifugo hasa wakati huu ambapo mitihani ya kitaifa inakaribia.

“Huu ni muhula ambao mitihani ya kitaifa inafanyika. Tunahimiza serikali kuzidisha doria za kiusalama maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama ili wanafunzi wasitatizike wanapojiandaa kufanya mitihani yao.” Alisema.