UTAMADUNI WATAJWA KUWA KIZINGITI KATIKA KUAFIKIWA USAWA WA KIJINSIA POKOT MAGHARIBI.
Tamaduni na imani za kijamii pamoja na siasa zimesalia changamoto kuu katika juhudi za kuafikiwa usawa wa kijinsia katika kaunti ya Pokot magharibi.
Akizungumza katika hafla ya kuwahamasisha wanahabari kuhusiana na swala la usawa wa jinsia iliyoandaliwa na shirika la village enterprise, mkurugenzi katika idara ya jinsia kaunti hiyo Emmanuel Oigwo alisema kwamba jamii haijakumbatia swala la usawa wa jinsia kutokana na kuendelea kushikilia imani ya kitamaduni kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii.
“Bado tunakabiliwa na changamoto ya imani ya kijamii katika kuafikia usawa wa kijinsia kaunti hii ya Pokot magharibi. Wengi bado wanaamini kwamba mwanamme ndiye anayefaa kupewa kipau mbele ila si mwanamke, kwa hivyo ukijaribu kuwafunza kuhusiana na swala la usawa wa jinsia wengi wanaona kwamba unawafunza wanawake kukosa heshima.” Alisema Oigwo.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na afisa katika shirika la SICOM Winnie Cheptoo ambaye alisema kwamba imani hizi zimechangia kuwepo visa vingi vya dhulumu za kijinsia kutokana na hali kwamba mwanamme amepewa kipau mbele katika jamii huku mwanamke akiwa hatambuliwi, akielezea umuhimu wa kuhusishwa wanahabari katika juhudi za kuafikiwa usawa wa jinsia.
“Jamii yetu inamthamini sana mwanamme zaidi ya mwanamke na swala hili limepelekea kukithiri visa vya dhuluma za kijinsia katika kaunti hii. Tumeona kuwahusisha wanahabari katika juhudi za kuafikia usawa wa jinsi itatusaidia sana.” Alisema Cheptoo.
Baadhi ya wanahabri ambao walishiriki shughuli hiyo walielezea umuhimu wake katika taaluma yao wakisema kwamba habari ambayo wamepata katika mafunzo hayo itasaidia kuhusu jinsi ya kuwasilisha ujumbe kwa jamii kuhusu swala zima la usawa wa jinsia bila ya kubuni mazingira ambayo huenda yakafanya isipokelewe vyema.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwetu kama wanahabari kwa kuwa yatatusaidia kufahamu jinsi ambavyo tutaweza kuzungumzia swala hili bila kuibua mazingira ambayo huenda yakapelekea kutopokelewa vyema na jamii.” Walisema.