OGWENO: VITA DHIDI YA UKEKETAJI ALALE VIMEFAULU PAKUBWA.
Msaidizi wa kamishina eneo la Alale kaunti ya Pokot magharibi Mourice Ogweno amesema kwamba visa vya ukeketaji eneo hilo vimepungua pakubwa hadi chini ya asilimia 5 mwaka huu.
Ogweno alisema kwamba tangu kuanza mwaka huu eneo hilo limeripoti kisa kimoja pekee cha ukeketaji juhudi hizo zikifanikishwa pakubwa na wadau mbali mbali ambao wamekuwa wakiendeleza uhamasisho miongoni mwa wananchi kuhusu athari za tamaduni hiyo.
Wakati uo huo Ogweno alisema maafisa wa polisi wamekuwa wakiendesha oparesheni dhidi ya tamaduni hiyo iliyopitwa na wakati ambapo ni mtu mmoja tu ambaye alinaswa akitekeleza shughuli hiyo na ambaye alikamatwa na kuchukuliwa hatua.
“Visa vya ukeketaji eneo hili vimepungua pakubwa hadi chini ya asilimia 5. Kuanzia mwezi januari mwaka huu kumeripotiwa tu kisa kimoja cha ukeketaji eneo hili. Hii ni hatua kubwa ambayo tumepiga eneo hili katika kukabili ukeketaji. Haya yameafikiwa kufuatia mchango wa wadau mbali mbali.” Alisema Ogweno.
Aidha Ogweno alisema kwamba wanaendeleza vikao na wananchi mara kwa mara kwa ushirikiano na shirika la world vision, hasa maeneo ambayo yalikuwa yakiendeleza awali shughuli hiyo kwa wingi akikiri kwamba juhudi hizo zimefaulu pakubwa.
“Tumekuwa tukiendeleza vikao vya umma kwa ushirikiano na shirika la world vision katika maeneo ambayo yamekuwa yakiripoti visa vingi vya ukeketaji hapo awali, na tumeona kwamba hatua hii imechangia pakubwa kupungua visa hivyo.” Alisema.