KINDIKI ALAUMIWA KWA KUENDELEA KUDORORA USALAMA MIPAKANI PA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.
Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kutoa shinikizo kwa waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kutimiza ahadi yake ya kuwaajiri maafisa wa NPR ili wasaidie katika kuleta usalama maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo.
Wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Seker Jane Mengich, viongozi hao walisema kwamba wahalifu ambao wamekuwa wakiendeleza uvamizi dhidi ya wakazi, wanafanya hivyo kwa kuwa wanafahamu kwamba kaunti hiyo ya Pokot magharibi haijapewa maafisa hao.
“Tunamwomba waziri Kindiki kwamba aharakishe mchakato wa kuajiri maafisa wa NPR katika kaunti hii ya Pokot magharibi ili tuwe sawa na kaunti zingine za bonde la Kerio. Wavamizi wamekuwa wakivamia kaunti hii kila mara kwa sababu wanafahamu sisi hatujapewa maafisa wa NPR.” Walisema.
Aidha viongozi hao walimtaka waziri Kindiki kutekeleza shughuli ya kuimarisha usalama bonde la Kerio kwa usawa, la sivyo serikali itwae bunduki ambazo ilikabidhi maafisa hao wa NPR katika kaunti za Turkana na Elgeyo Marakwet wanazodai kwamba zinatumika katika uvamizi huo.
“Waziri Kindiki alisema tumpe wiki moja kabla ya kutupa NPR ila tangu atoe ahadi hiyo hatujaona hatua yoyote ambayo imepigwa. Kwa hivyo tunamwambia iwapo hataajiri maafisa hao kaunti hii na kuwapa bunduki, basi zile ambazo maafisa wa NPR kaunti za Turkana na Elgeyo Marakwet walipewa zirudishwe.” Walisema.
Walitoa wito kwa wakazi wa maeneo ambayo yameathirika kwa uvamizi huo kutolipiza kisasi bali waendele kuishi kwa amani, na kuyasikiliza mawaidha ya wazee ili kuwe na mazingira salama ya viongozi kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha maendeleo yanaafikiwa.
“Tunawahimiza wakazi wa kaunti hii ambao wameathirika na uvamizi kutolipiza kisasi na badala yake kuendelea kudumisha amani, na kusikiliza mawaidha ya wazee wetu ili tupate nafasi ya kutekeleza maendeleo inavyopasa.” Walisema.