VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAONYWA DHIDI YA KUJIHUSISHA NA SIASA ZA MAPEMA.

Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ni kiongozi wa hivi punde kuwasuta viongozi ambao wanaendeleza siasa za mwaka 2027 mwaka mmoja tu tangu taifa kutoka kwenye msimu wa siasa za uchaguzi.

Komole alisema kwamba sasa ni wakati ambapo viongozi wa kisiasa wanapasa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba maswala ambayo yanawakumba wananchi ikiwemo hali ya usalama hasa maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo yanashughulikiwa.

Alisema kama viongozi wa kaunti hiyo kamwe hawataruhusu baadhi ya wanasiasa kuvuruga mipango ya maendeleo ambayo wanakusudia kutekeleza kwa ajili ya wakazi kwa kujihusisha na siasa za mapema.

“Siasa za mapema katika kaunti hii tumekataa kwa sababu haziwezi kuwasaidia wananchi. Sisi hapa tunataka kuwahudumia wananchi katika mazingira tulivu. Tukianza mambo ya siasa wakati huu itakuwa vigumu kukutana pamoja kushughulikia maswala yanayowakumbva wananchi kama vile utovu wa usalama.” Alisema Komole.

Komole alisema kwamba japo ni haki ya kila mmoja kuendeleza siasa wakati anaoona kwamba ni bora kufanya hivyo, siaza za mapema zitaleta migawanyiko miongoni mwa viongozi na wananchi na hivyo kufanya vigumu kutekeleza mipango ya maendeleo ya serikali.

“Kila mtu ana haki yake ya kufanya siasa wakati wowote. Lakini sasa iwapo tutaanza siasa tutaleta migawanyiko miongoni mwa wananchi. Kila mtu sasa mawazo yake yatakuwa tu ya kisiasa na hakuna jinsi utafanya kazi. Hivyo siasa za mapema si nzuri kwa maendeleo.” Alisema.