ONYANCHA: MASOMO YA SEKONDARI YA MSINGI YAMEFAULU PAKUBWA KIPKOMO.

Shughuli za masomo katika shule ya sekondari ya msingi eneo la Kipkomo, pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi zinaendelea vyema kulingana na matarajio.

Haya ni kulingana na mkurugenzi wa elimu eneo hilo Evans Onyancha ambaye alisema kwamba mikakati ambayo iliwekwa kuhakikisha kwamba masomo katika shule hizo yanafaulu imeendelea kutekelezwa na kwamba kufikia sasa, hapajashuhudiwa changamoto kubwa katika utekelezwaji wake.

Onyancha aliwapongeza wakuu wa shule hizo kwa juhudi ambazo wanafanya kuhakikisha kwamba masomo katika shule hizo yanaendelea inavyokusudiwa.

“Masomo ya shule za sekondari ya msingi yameendelea vyema eneo hili tangu yalipoanzishwa. Serikali ilitupa walimu kwa shule hizo, madarasa pia yamejengwa na sasa walimu wameukumbatia vyema mfumo huo wa elimu.” Alisema Onyancha.

Wakati uo huo Onyancha alisema kwamba ushirikiano uliopo miongoni mwa wadau wa elimu eneo hilo umepelekea wakuu wa shule kuwa na wakati mzuri wa kutekeleza shughuli zao, na kupelekea matumizi bora ya fedha ambazo zinatolewa kwa shule na serikali.

“Kuna ushirikiano mzuri baina ya wadau wa elimu katika eneo hili. Hali hii imefanya wakuu wa shule kupata wakati mzuri wa kuendeleza shughuli shuleni hali ambayo imechangia pakubwa matumizi bora ya fedha ambazo zinatolewa shuleni na serikali.” Alisema.