IDARA YA USALAMA KIPKOMO YAONYA VIKALI DHIDI YA BIASHARA YA MIHADARATI NA POMBE HARAMU.
Idara ya usalama eneo la Kipkomo eneo bunge la Pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi imeapa kukabili biashara ya mihadarati eneo hilo kuhakikisha kwamba inamalizwa kabisa.
Hii ni baada ya maafisa wa usalama kwa msaada wa wakazi wa eneo hilo kugundua bangi iliyokuwa imepandwa katika shamba la mkulima mmoja kabla yao kung’oa bangi hiyo na kisha kumtia nguvuni mshukiwa.
Naibu kamishina eneo la Kipkomo George Chege alitoa onyo kali kwa wanaoendeleza biashara hiyo kwamba watakabiliwa vikali kulingana na sheria.
“Maafisa wetu wanaofanya kazi kwa karibu sana na wakazi wa eneo hilo walipata taarifa kwamba kuna mkulima mmoja ambaye alikuwa amepanda bangi shambani mwake. Tulienda tukang’oa bangi hiyo na kumtia nguvuni mhusika. Sasa nawaonya wale wote ambao wanaendeleza biashara hii ya mihadarati kwamba tupo macho na tutawakabili vilivyo.” Alisema Chege.
Wakati uo huo Chege alisema kwamba kwa ushirikiano na machifu, manaibu chifu na wakazi wa eneo hilo wataendeleza vita dhidi ya ugemaji wa pombe haramu ili kuhakikisha kwamba wakazi wanajihusisha na biashara halali.
“Nawaonya pia wale ambao wanaendeleza biashara ya pombe haramu kwamba tutawaandama. Tunataka wananchi wetu hapa kuishi bila matatizo ya pombe. Tutashirikiana na wananchi, machifu na manaibu wao pamoja na vitengo vyote vya usalama kuhakikisha biashara hii inakomeshwa.” Alisema.