SERIKALI YATAKIWA KUENDELEZA MPANGO WA LISHE SHULENI ILI KUKABILI UTAPIA MLO NA KUWAVUTIA WANAFUNZI SHULENI, SARMACH.

Visa vya utapiamlo vimekithiri eneo la Sarmach eneo bunge la Sigor kaunti ya Pokot magharibi kufuatia baa la njaa ambalo linawakabili wakazi wengi wa eneo hilo.

Haya ni kulingana na mkurugenzi wa shirika la amani la KEPACO, Kenya pastoralists community organization Diana Rotich ambaye amesema kwa ushirikiana na wahudumu wa afya wanapania kupeleka msaada eneo hilo ukijumuisha chakula na matibabu kwa watoto walioathirika.

“Visa vya utapia mlo vipo juu sana eneo la Sarmach huko pokot ya kati kufuati tatizo la chakula. Ndio maana sisi kama shirika tumeshirikiana na wahudumu wa afya kutoka hapa Makutano na Kapenguria ili twende kuwashughulikia wakazi hao kwa kuwapa chakula na huduma za matibabu.” Alisema Rotich.

Aidha Rotich alisema kwamba swala la elimu eneo hilo limekuwa changamoto kuu kutokana na hali kwamba shule zilizopo ziko mbali, akitaka serikali kujenga shule na kuanzisha mpango wa lishe shuleni ambao utawavutia wanafunzi wengi kuhudhuria masomo.

“Kuna haja ya kujenga shule eneo hilo kwa sababu viwango vya elimu vipo chini sana kutokana na hali kwamba shule zipo mbali. Pia ningehimiza serikali kuendeleza mpango wa lishe shuleni ili kuwavutia wananchi zaidi shuleni.” Alisema.

Wakati uo huo Rotich alielezea haja ya wakazi wa maeneo hayo kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ili kuwawezesha kujizuia kukata miti kwa ajili ya uchomaji makaa, hali ambayo amesema imechangia pakubwa ukame ambao unashuhudiwa eneo hilo.

“Pia kuna tatizo la mazingira ambapo watu wamekata miti sana ili kuchoma makaa hali ambayo imepelekea ukame eneo hilo. Tunalenga pia kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema.