WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHAKIKISHIWA MAJI SAFI YA MATUMIZI.

Waziri wa maji katika kaunti ya Pokot magharibi Lucky Litole amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba wizara yake inaendeleza mikakati ya kuhakikisha wanapata maji safi ya matumizi.

Litole alisema kwamba serikali kupitia wizara yake imeendeleza uchimbaji wa visima ambavyo vinatarajiwa kuwekwa mitambo ya sola pamoja na mabomba ambayo yatafanikisha juhudi za kuhakikisha kila nyumba inapata maji safi.

Wakati uo huo Litole alisema serikali ipo katika awamu ya mwisho ya mradi wa maji wa murunyi na hivi karibuni takriban nyumba 650 kaunti hiyo zitaweza kunufaika na maji safi kupitia mradi huo.

“Hakikisho langu kwa wananchi ni kwamba hivi karibuni wataweza kupata maji safi katika nyumba zao. Mwaka jana tulichimba mabwawa mengi na sasa tunalenga kuweka mitambo ya sola na mabomba ambayo yatawawezesha wananchi kupata maji.” Alisema Litole.

Aidha Litole alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kushiriki kwa wingi katika zoezi la upanzi wa miti pamoja na kuhakikisha wanatunza miche wanayopanda katika juhudi za kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

“Naomba kwamba sote tushirikiane katika shughuli ya upanzi wa miti. Na tunapopanda miche tuhakikishe kwamba tunaitunza ili tukabili mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema.