WAZAZI WATAKIWA KUWATUNZA VYEMA WANAO WANAPOREJEA NYUMBANI KWA LIKIZO.
Wanafunzi wanaporejea nyumbani kwa likizo baada ya kukamilika muhula wa pili, miito imeendelea kutolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya ulezi kuhakikisha wanafunzi wanasalia salama.
Baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Mnagei Richard Todosia na mwenzake wa Kapenguria Richard Mastaluk walisema kwamba ni jukumu la wazazi kuhakikisha kwamba wanao wanasalia salama ili warejee shuleni baada ya kukamilika likizo wakiwa katika hali nzuri.
Aidha viongozi hao waliwataka wazazi kuwahusisha wanao katika shughuli mbali mbali ili wasipate wakati wa kijihusisha na mambo ambayo huenda yakaathiri elimu yao.
“Tunawahimiza wazazi kuwa makini na wanao wanaporejea nyumbani kwa likizo ya mwezi agosti na kuhakikisha kwamba wanawatunza vyema. Wawahusishe katika shughuli mbali mbali hapo nyumbani ili wanaporejea shuleni baada ya likizo, wawe katika hali nzuri ya kuendeleza masomo.” Walisema.
Waliwaonya vikali wazazi dhidi ya kuwaoza mapema watoto wao wakisema kwa ushirikiano na wadau wa usalama wanaweka mikakati ya kuhakikisha kila mwanafunzi anakamilisha masomo kabla ya kujihusisha na maswala ya ndoa.
“Tunatoa onyo kwa wazazi wote kaunti hii dhidi ya kujaribu kuwaoza watoto wao kabla ya kukamilisha masomo yao. Tunaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anakamilisha masomo yake hadi chuo kikuu kabla ya kuhusishwa kwenye maswala ya ndoa.” Walisema.