HATUA YA KUBUNIWA KAMATI ITAKAYOONGOZA MAZUNGUMZO BAINA YA SERIKALI NA UPINZANI YAPOKEA PINGAMIZI.
Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wametofautiana vikali na hatua ya kubuniwa kamati ya wanachama kumi itakayoongoza mazungumzo baina ya serikali ya Kenya kwanza na upinzani chini ya uongozi wa aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.
Kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Pokot magharibi Martine Komongiro alisema kwamba maswala ambayo wanashinikiza viongozi wa azimio ikiwemo kupunguzwa gharama ya maisha yamo kwenye ajenda ya serikali ya Kenya kwanza na tayari rais William Ruto anayashughulikia.
Komongiro alisema kwamba kubuniwa kamati hiyo kushughulikia maswala ambayo yaliibuliwa na azimio ni kupoteza muda kwani wakenya walikuwa na imani na rais William Ruto kwa kumchagua katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti mwaka jana.
“Maswala ambayo upinzani inashinikiza kujadiliwa katika kamati ya watu kumi ambayo inaongozwa na aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo tayari yapo kwenye ajenda ya Kenya kwanza. Hivyo sioni haja ya kubuniwa kamati hii wakati wakenya walikuwa na imani na Ruto kuwa rais.” Alisema Komong’iro.
Komongiro alimtaka rais William Ruto kutokubali kushawishiwa kuandaa mazungumzo na viongozi wa upinzani akidai hii ni mbinu ya upinzani kuhakikisha kwamba serikali haitekelezi maendeleo ilivyowaahidi wakenya ili wapate sababu ya kuwachochea wakenya kutompigia kura tena rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
“Namsihi rais Ruto kwamba asikubali kupoteza muda kwa kamati kama hizi. Sasa ni wakati ambapo anafaa kutumia muda wake kuwatimizia wakenya ahadi alizotoa wakati wa kampeni. Tunajua hizi ni mbinu za upinzani kuhujumu maendeleo ili wapate sababu ya kuwachochea wakenya kutompigia tena Ruto kura katika uchaguzi mkuu ujao.” Alisema.