IDARA YA USALAMA POKOT MAGHARIBI YAELEZEA MAFANIKIO DHIDI YA WEZI WA MIFUGO.
Idara ya usalama katika kaunti ya Pokot magharibi imewahakikishia wakazi kwamba usalama umeimarishwa hasa maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama unaosababishwa na wezi wa mifugo.
Akizungumza afisini mwake mjini Kapenguria kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam alisema kwamba idadi ya maafisa wa polisi imeongezwa katika maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo ili kuhakikisha kwamba doria ya kiusalama inaimarishwa.
Aidha Katam alielezea matumaini kwamba maeneo ambayo yamekuwa sugu katika swala la utovu wa usalama ikiwemo Kainuk na lami nyeusi sasa yameanza kushuhudia usalama kufuatia oparesheni ya maafisa wa polisi ambayo inaendelezwa.
“Nawahakikishia wananchi kwamba tumeimarisha usalama katika kaunti hii hasa maeneo ya mipakani ambako kumekuwa tatizo kwa muda sasa. Tumeongeza idadi ya maafisa wa polisi, na nina furaha kwa sababu sasa maeneo ambayo yamekuwa sugu kwa tatizo la usalama kama vile lami nyeusi sasa ni salama.” Alisema Katam.
Hata hivyo Katam alitaja eneo la Ombolion kuwa moja ya maeneo ambayo yangali yanashuhudia visa vya uvamizi akitoa hakikisho kwa wakazi kwamba mikakati inaendelezwa na idara ya usalama kuhakikisha visa hivyo vinakabiliwa na kumalizwa.
“Kwa sasa kama idara ya usalama tunaendeleza mikakati kuhakikisha kwamba eneo la Ombolion pia linakuwa salama kwa sababu sasa ni eneo hilo tu ambalo linatusumbua.” Alisema.
Hivi majuzi mtu mmoja aliuliwa kwa risasi eneo hilo la Ombolion baada ya wavamizi waliokuwa wamejificha kichakani kuvamia gari moja la abiria lililokuwa likisafiri kutoka Romos na kuanza kulimiminia risasi.