KACHAPIN: MAPENDEKEZO YA JOPO LA KUANGAZIA MAGEUZI YA ELIMU YATAIMARISHA SEKTA YA ELIMU NCHINI.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza mapendekezo ya jopo lililobuniwa na rais William Ruto kuangazia mageuzi katika sekta ya elimu nchini chini ya uwenyekiti wa Prof. Raphael Munavu.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Kaisagat alikotoa fedha za ujenzi wa madarasa, Kachapin alisema mabadiliko ambayo yamependekezwa na jopo hilo kwenye mtaala mpya wa elimu CBC yatasaidia pakubwa taifa kuhusu swala la ajira ikizingatiwa unazingatia pakubwa ubunifu miongoni mwa wanafunzi.

“Yale mabadiliko ambayo yamependekezwa katika CBC yatasaidia pakubwa taifa letu hasa katika swala la ajira iwapo yatatekelezwa vizuri, ikizingatiwa kwamba mfumo huu unazingatia pakubwa ubunifu miongoni mwa wanafunzi.” Alisema Kachapin.

Wakati uo huo Kachapin alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau katika sekta ya elimu kwamba serikali yake itashirikiana kikamilifu na serikali kuu kuhakikisha miundo msingi bora kwenye shule za kaunti hiyo ili kutoa mazingira bora kwa shughuli za elimu.

“Mwaka huu tumetenga zaidi ya milioni 700 ambapo kila mtoto atapata zaidi ya alfu 25 kwa walio katika shule za mabweni na alfu 11 kwa wanafunzi wa kutwa. Sisi kama serikali ya kaunti tunashirikiana kikamilifu na serikali kuu kuona kuwa shule zetu zinajengwa.” Alisema.

Baadhi ya viongozi walioandamana na gavana Kachapin kwenye hafla hiyo wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Siyoi Esther Serem walimpongeza Kachapin kwa kujitolea katika kuimarisha sekta ya elimu, wakitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanafunzi kutia bidii masomoni.

“Tunampongeza gavana kwa kujitolea kuhakikisha kwamba sekta ya elimu kaunti hii inaimarishwa. Sasa ni jukumu la wanafunzi kuhakikisha kwamba wanatia bidii masomoni kwa kuwa bila elimu hawataweza kufika mbali.” Walisema.