MTU MMOJA AUAWA KATIKA SHAMBULIZI LA HIVI PUNDE MPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA.
Taharuki imeendelea kutanda katika mpaka wa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana baada ya mtu mmoja kuuliwa kwa risasi eneo la Ombolion na watu wanaoaminika kuwa wavamizi kutoka kaunti jirani, jumanne mchana.
Inaarifiwa wavamizi hao walivamia gari lililokuwa likisafiri kutoka Romos na kulimiminia risasi ambapo abiria mmoja aliuliwa huku wengine wakinusurika.
Akithibitisha kisa hicho chifu wa Ombolion Joseph Korkimul alisema kwamba wavamizi hao waliweka vizuizi barabarani na kujificha vichakani kabla ya kuvamia gari hilo lililokuwa likijaribu kuvuka vuzuizi hivyo.
“Wavamizi kutoka kaunti jirani waliweka vizuizi kwenye barabara ya kutoka Romos hadi Turkwel na kisha kujificha vichakani. Wakati gari hilo likijaribu kuvuka vizuizi hivyo ndipo walitokezea na kuanza kulimiminia risasi ambapo mtu mmoja aliaga dunia.” Alisema Korkimul.
Korkimul alikiri kuwa eneo hilo limekuwa likishuhudia visa vya utovu wa usalama mara kwa mara na kwamba linahitaji maafisa zaidi wa akiba NPR ambao watasaidiana na maafisa wa usalama kuimarisha doria.
Kwa upande wake naibu kamishina eneo la pokot kaskazini James Ajuang alisema kwamba maafisa wa polisi wameongezwa eneo hilo ili kuimarisha usalama.
“Maafisa wa polisi wametumwa katika eneo hilo kuimarisha doria huku wakijaribu kuwafuata wavamizi ambao walitekeleza mauaji hayo.” Alisema Ajuang.
Ni kisa ambacho kimeshutumiwa vikali na viongozi kaunti ya Pokot magharibi wakiongozwa na seneta Julius Murgor ambao aidha waliitaka serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani ya nchi kuharakisha zoezi la kuwaajiri maafisa zaidi wa NPR watakaosaidia katika kuimarisha hali ya usalama.
Aidha Murgor alitoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kudumisha amani na kusitisha visa vya uvamizi ambao umepelekea mauaji ya wakazi wengi huku wengine wakilazimika kuyahama makazi yao kwa hofu ya kuvamiwa.
“Nawaomba wakazi wa maeneo hayo kusitisha maswala ya uvamizi na kuishi kwa amani ili kutoa nafasi ya kutekelezwa maendeleo pamoja na watoto wetu kupata nafasi ya kuhudhuria masomo shuleni.” Alisema Murgor.
Mwezi uliopita waziri wa maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki alizuru eneo la Turkwel akiahidi kuhakikisha kwamba hali ya usalama inaimarishwa kwa kuwaajiri maafisa zaidi wa NPR, pamoja na kufungua barabara zaidi za kiusalama.