USALAMA WAIMARISHWA KWENYE MISITU YA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI KUZUIA UKATAJI MITI HARAMU BAADA YA RAIS KUONDOA MARUFUKU.

Idara ya misitu katika kaunti ya Pokot magharibi imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba hamna ukataji miti ulio kinyume cha sheria baada ya rais William Ruto kuondoa marufuku iliyowekwa dhidi ya shughuli hiyo na uongozi uliotangulia.

Akizungumza na wanahabari afisa anayesimamia misitu kaunti hiyo Fredrick Atanus Ashiono alisema japo hamna ukataji miti ulio kinyume cha sheria ambao umeripotiwa hadi kufikia sasa, idara hiyo imezidisha ulinzi wa misitu kwa kuweka maafisa wa polisi zaidi.

Hata hivyo Ashiono alielezea changamoto wanayokumbana nayo dhidi ya wakazi ambao wamevamia misitu hiyo kwa kuendeza shughuli za kilimo hali aliyosema kwamba inaathiri maeneo ya chemchemi akiahidi kuhakikisha hali hiyo inashughulikiwa.

“Rais alipotoa marufuku ya ukataji miti kwenye misitu nchini hatujapata uhalifu wowote kwenye misitu yetu. Idadi kubwa ya misitu kwenye kaunti hii ni ya kiasili, na tumeweka mikakati kuhakikisha kwamba inalindwa inavyofaa. Tunakabiliwa na changamoto moja tu ya wakazi kuvamia misitu hiyo na kupanda mimea hali ambayo inaathiri maeneo ya chemchemi.” Alisema Ashiono.

Wakati uo huo Ashiono alisema wanaendeleza juhudi za kuhakikisha idadi ya misitu kaunti hiyo inafikia asilimia 30 akitoa wito kwa wadau mbali mbali kushirikiana na idara hiyo kuhakikisha kwamba hilo linaafikiwa kwa kupanda miche milioni 14.9 kila mwaka.

Aidha aliwahimiza wakazi kuhakikisha kwamba wanatunza miche wanayopanda katika juhudi za kuafikia malengo hayo.

“Katika kaunti hii tuna asilimia 20.1 ya misitu na tunahitajika kuongeza misitu hiyo ili ifikie asilimia 30. Sasa hivi tunahimiza wadau kushirikiana nasi ili tuweze kuafikia malengo hayo kwa kupanda miche milioni 14.9 kila mwaka.” Alisema.