RAILA ATAKIWA KUSTAAFU SIASANI NA KUKOMA KUWA TATIZO KWA UONGOZI WA TAIFA.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kumshutumu kinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga kwa kile wamedai kwamba ameendelea kuwa tatizo kwa serikali kwa miaka mingi kupitia maandamano.

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alimsuta Raila kwa kile alisema kwamba  kutumia mbinu moja kwa miaka mingi hali mwenyewe hana suluhu kwa matatizo ambayo yanakumba taifa, akimtaka kujitenga na harakati hizo na kustaafu kwa amani ili aheshimike kwa mchango wake kwa taifa hili.

Wakati uo huo Lochakapong alitaka kuchukuliwa hatua za kisheria viongozi wa upinzani ambao wamekuwa na mazoea ya kuitisha maandamano nchini ambayo yamepelekea uharibifu wa mali na hata kusababisha kupoteza maisha baadhi ya wananchi.

“Haya ni maswala ambayo hayawezi kutusaidia. Mtu mmoja tu ametatiza watu Kenya hii kila wakati na najua kwamba hata yeye hana suluhu kwa matatizo ambayo yakumba taifa hili. Namshauri Raila kwamba astaafu vizuri kama mzee wa taifa hili na ataheshimika kwa mchango wake nchini.” Alisema Lochakapong.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi ya Masol Wilson Chekeruk ambaye aidha alimsuta mbunge wa Pokot kusini David Pkosing kwa kwenda kinyume na viongozi wa kaunti hiyo na kuunga mkono sera za viongozi wa upinzani akisisitiza kwamba maandamano hayo hayataleta suluhu kwa gharama ya juu ya maisha.

“Kuna kiongozi mmoja ambaye naona ni kama shetani amemwingia na anataka kuiga tabia ya watu ambao si wa eneo hili. Licha kusema gharama ya maisha imepanda, hakuna suluhu katika kuandaa maandamano ambayo yanapelekea kuharibiwa mali ya wananchi.” Alisema Chekeruk.