VIJANA WATAKIWA KUWA MSITARI WA MBELE KATIKA KUDUMISHA AMANI KASKAZINI MWA BONDE LA UFA.
Wito umetolewa kwa vijana katika kaunti 6 za kaskazini mwa bonde la ufa ikiwemo kaunti ya Pokot magharibi kujitokeza na kuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kwamba amani inadumishwa katika kaunti za kanda hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shirika la amani la Kepako, mwanzilishi wa shirika hilo Diana Rotich alisema kwamba vijana ndio mara nyingi hutumika vibaya katika mswala ya kutatiza amani ikiwemo wizi wa mifugo pamoja na maswala ya maandamano na sasa ni jukumu lao kuhakikisha hayo yanakomeshwa kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi ya seker Jane Mengich.
“Tunataka amani katika kaunti zetu sita na sisi kama vijana tumeonelea ni wakati ambapo tunapasa kujitokeza na kusema lazima amani idumu, Kwa sababu ni sisi vijana ambao mara nyingi hutumika katika wizi wa mifugo na hata maswala kama maandamano.” Alisema Rotich.
Aliyekuwa mbunge wa cherang’ani Wesley Korir miongoni mwa viongozi walioalikwa katika hafla hiyo alisema kuwapokonya wahalifu silaha si suluhu ya kudumu kwa tatizo la usalama bali serikali inapasa kubuni njia ya kuwasaidia wale ambao wamekuwa wakijihusisha na wizi wa mifugo ili kuhakikisha kwamba wanajitenga na hulka hiyo kabisa.
“Tumekuwa tukijaribu kupokonya silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wananchi lakini hii haisaidii. Kwa hivyo tunapasa kutafuta njia mbadala ambapo tunapasa kubuni njia ya kuwasaidia vijana hawa na njia moja ni kupitia michezo. Kaunti hii ina talanta nyingi sana.” Alisema Korir.
Kwa upande wake kaimu naibu kamishina kaunti ya Pokot magharibi David Bowen alisema idara ya usalama katika kaunti hiyo inafanya iwezalo kwa ushirikiano na jamii kuhakikisha amani inadumishwa huku afisa katika idara ya michezo na utamaduni Reuben Lokipenet akitoa wito kwa kaunti hizo kuhakikisha amani inadumishwa ili kuafikiwa maendeleo.
“Sehemu ya Pokot magharibi tuna amani japo maeneo ya mipaka ndiyo tunayojaribu kufanya tuwezalo kuhakikisha kwamba amani inadumu kwa kuhusisha jamii katika juhudi hizi. Tunataka kaunti jirani kuzingatia amani ili kuafikiwe maendeleo maeneo haya.” Walisema.