LOCHAKAPONG AAHIDI KUIMARISHA HALI YA WADI YA MASOL ENEO BUNGE LA SIGOR.

Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ameahidi kuhakikisha kwamba anaimarisha hali katika wadi ya Masol eneo bunge hilo ambayo ametaja kuwa moja ya maeneo ambayo yametengwa kwa muda kwa maswala ya maendeleo.

Akizungumza katika kijiji cha Cheptembur katika hafla ya kuwarudishia wakazi wa wadi hiyo shukrani kwa kumchagua tena mbunge, Lochakapong alisema kwamba kwa ushirikiano na mwakilishi wadi wa eneo hilo atahakikisha kwamba anachimba visima ili kukabili tatizo la maji ambalo ndiyo changamoto kuu eneo hilo miongoni mwa maswala mengine.

“Tumekuwa na changamoto kubwa ya maji eneo hili na watu wanalazimika kwenda mbali sana kupata maji. Mimi kwa ushirikiano na mwakilishi wadi wa eneo hili tutahakikisha kwamba tunachimba visima ili kuhakikisha wakazi wanapata maji ya kutosha.” Alisema Lochakapong.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi ya eneo hilo Wilson Chekeruk ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge la kaunti ya bajeti na ambaye alisema kwamba punde bajeti ya kipindi cha fedha cha mwaka 2023/2024 itakapoanza kutekelezwa eneo hilo litanufaika pakubwa kimaendeleo.

“Zipo changamoto nyingi sana ikiwemo barabara na maji. Lakini sasa mimi kama mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni nitahakikisha kwamba eneo hili linapata miradi mingi ya maendeleo pindi tu bajeti itakapoanza kutekelezwa.” Alisema Chekeruk.

Kauli za viongozi hao zilijiri wakati ambapo wakazi wamelalamikia pakubwa athari za kiangazi wanachosema kuwa kinachangia pakubwa hali ya utovu wa usalama, wakitaka serikali kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji mashamba ili wapate nafasi ya kupanda chakula.

“Tumeathirika sana hasa kutokana na swala la ukame. Iwapo serikali ingetusaidia kwa kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji mashamba ili tupate chakula cha kutosha, swala la utovu wa usalama lingekabiliwa pakubwa eneo hili.” Walisema.