KACHAPIN ASIFIA MFUMO WA UGATUZI KUWA CHANZO CHA MAENDELEO MASHINANI.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza pakubwa mfumo wa ugatuzi akisema kwamba umepelekea kuafikiwa maendeleo makubwa maeneo ya mashinani ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo serikali ya kitaifa pekee ilikuwa ikiendesha shughuli zote.

Akizungumza wakati alipokagua miradi katika hospitali za Orolwo na Kacheliba pamoja na kuzindua rasmi chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Kacheliba, Kachapin aliwakosoa vikali wanaosema kwamba mfumo wa ugatuzi haujaleta manufaa katika taifa hili.

Wakati uo huo Kachapin alisema kwamba uzinduzi wa chumba cha upasuaji katika hospitali hiyo pamoja na kinachotarajiwa eneo la Sigor utarahisisha huduma na kupunguza msongamano katika hospitali ya Kapenguria.

“Tumezindua chumba cha upasuaji katika hospitali ya Kacheliba pamoja na chumba cha kujifungua katika hospitali ya Orolwo. Hii miradi nilianza mwaka 2013 na nimekuja kukamilisha. Haya ni baadhi ya mafanikio ya mfumo wa ugatuzi. Nawakosoa wale wanaosema kwamba ugatuzi haufanyi kazi.” Alisema Kachapin.

Mwakilishi wadi ya Soak ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Pokot magharibi Martine Komongiro alimsuta aliyekuwa gavana John Longapuo kwa kutelekeza miradi hiyo iliyokuwa imeanzishwa na gavana Kachapin katika awamu yake ya kwanza akisema hatua hiyo haikustahili.

“Naikashifu serikali iliyotangulia kwa sababu waliona kwamba hii miradi ilikuwa ya mtu binafsi na kuitelekeza. Haistahili kwa mtu yeyote kutelekeza miradi ambayo imegharimu pesa nyingi za mlipa ushuru kwa sababu tu za tofauti za kisiasa na mpinzani wake.” Alisema Komong’iro.

Wakazi wa eneo la Orolwo walimpongeza gavana Kachapin kwa kufungua chumba cha kujifungua kina mama katika hospitali ya Orolwo wakisema kwamba hatua hiyo sasa itawapunguzia mwendo mrefu pamoja na gharama ya kutafuta huduma hizo kwingine.

“Namshukuru sana gavana kwa kujenga chumba cha kujifungua hapa. Hatua hii sasa itatupunguzia gharama na safari ya mwendo mrefu kutafuta huduma hizo sehemu nyingine.” Walisema.