OCS WA KONGELAI ASUTWA KWA KUWA KIKWAZO KATIKA JUHUDI ZA KUHAKIKISHA USALAMA WA WAKAZI.
Mzee wa kijiji cha Simotwo eneo la Kongelai kaunti ya Pokot magharibi Johnson Lodepa ameelezea wasi wasi kuhusiana na usalama wa eneo hilo kutokana na kuwepo kundi la vijana ambao hawajulikani walikotoka.
Lodepa alisema kwamba vijana hao zaidi ya 8 na ambao wanaishi katika chumba kimoja huonekana tu nyakati za usiku na haijulikani wanachofanya eneo hilo.
Alisema kwamba la kutia hofu zaidi, juhudi za kumtaka OCS wa eneo hilo kuwachunguza vijana hao zimekuwa zikiambulia patupu kwani hamna hatua yoyote ambayo imechukuliwa hadi kufikia sasa.
“Kuna vijana hapa ambao sijui walitoka wapi, na vijana hawa wanaishi kwa nyumba moja zaidi ya wanane. Na wao hawaonekani nyakati za mchana. Ni usiku tu ndio utawaona wanatembea tembea huku, na hawajulikani kazi wanayofanya. Ila tatizo ni kwamba tumejaribu kumwambia OCS wa eneo hili lakini hamna hatua ambayo anachukua. Sasa tunaishi kwa wasiwasi sana huku.” Alisema Lodepa.
Wakati uo huo Lodepa alidai kwamba afisa huyo amekuwa akilemaza juhudi za kukabili ugemaji wa pombe eneo hilo kwa kile amedai kwamba anashirikiana na wakazi wanaohusika biashara hiyo haramu.
“Huyu OCS amekuwa kikwazo kikubwa sana katika kukabili ugemaji wa pombe haramu huku. Kuna wakati pombe ilinaswa ikapelekwa kwenye kituo cha polisi ila OCS mwenyewe akairudisha pombe hiyo. Na sasa amekuwa akishirikiana na wagemaji wa pombe hali ambayo imekuwa vigumu kukabiliana nao.” Alisema.