VIONGOZI WA KENYA KWANZA WAKASHIFU MAANDAMANO YA MRENGO WA AZIMIO.

Viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi wanaoegemea mrengo wa Kenya kwanza wameshutumu vikali maandamano yaliyoendeshwa na mrengo wa azimio katika kuadhimisha siku ya sabasaba ijumaa iliyopita kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha.

Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao waliutaka muungano wa azimio kutumia njia zinazostahili ikiwemo bunge la kitaifa kushinikiza maswala mbali mbali wala si njia za kuharibu mali ya wananchi.

Aidha viongozi hao walimsuta kinara wa azimio Raila Odinga kwa kutangaza kuanzisha mchakato wa kukusanya sahihi za kumtoa rais William Ruto afisini, wakimtaka kukubali uamuzi wa wakenya na kusubiri hadi uchaguzi mkuu ujao ili kurejea uwanjani.

“Mimi sioni haja ya kusema watu waandamane kwa sasa. Kuna njia nyingi za kutumia kuafikia yale ambayo muungano wa azimio unashinikiza. Kuna wabunge wengi sana wa azimio kwenye bunge. Watumie bunge kushinikiza hayo.” Walisema.

Viongozi hao walitoa wito kwa kiongozi wa azimio Raila Odinga kutovuruga heshima aliyo nayo nchini kufuatia juhudi alizofanya kuafikiwa demokrasia, na badala yake kukumbatia mazungumzo ambayo yatapelekea kulipelekea taifa mbele na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.

“Tunamheshimu Raila sana kutokana na maswala mengi ambayo amepigania taifa hili. Kwa hivyo hapasi kuvuruga heshima ambayo ako nayo nchini. Akumbatie mazungumzo ambayo yatasaidia taifa kusonga mbele.” Walisema.