KIWANDA CHA SIMITI CHA SEBIT CHAAHIDI KUTENGA ASILIMIA 80 YA NAFASI ZA AJIRA KWA WAKAZI WA POKOT MAGHARIBI.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amempongeza mwekezaji ambaye anaendeleza ujenzi wa kiwanda cha simiti eneo la Sebit eneo bunge la Pokot kusini anachosema kitakuwa cha manufaa makubwa kwa kaunti hiyo.

Akizungumza alipokutana na mwekezaji huyo ambaye ni mwenyekiti wa kampuni za Devki Arawal Guru afisini mwake, gavana kachapin alisema kwamba mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 45 utachangia pakubwa katika kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo.

“Sisi kama kaunti ya Pokot magharibi tunafurahia sana miradi kubwa kama huu wa simiti eneo la Sebit kwa sababu tunafahamu kuwa ni sisi ndio tutakaonufaika pakubwa. Uchumi wetu utaweza kuimarika kwa haraka kufuatia uwekezaji kama huu.” Alisema Kachapin.

Kachapin alisema kwamba kiwanda hicho kimetoa ajira kwa vijana wengi, huku akiahidi kwamba serikali yake itatoa mazingira bora kwa wawekezaji zaidi kutekeleza shughuli zao katika kaunti ya Pokot magharibi.

“Kwa sasa wanaoajiriwa ni zaidi ya watu 900 kila siku. Hii ina maana kwamba wakati kiwanda hicho kitaanza kufanya kazi vijana wetu wengi wataajiriwa. Na hili ndilo tunalohitaji kama wananchi wa Kenya. Serikali yangu itawapa mazingira bora wawekezaji wote kutekeleza shughuli zao ili watu wetu pia wanufaike.” Alisema.

Kwa upande wake Guru alisema  kwamba mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo utabuni nafasi za ajira kwa watu takriban alfu 2 huku asilimia 80 ya watakaoajiriwa wakiwa wakazi wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi.

“Kiwanda hiki kitakamilika katika kipindi cha miezi miwili au mitatu ijayo. Na kitakapokamilika tutaajiri zaidi ya watu alfu 2 kuhudumu hapo, asilimia 80 ya ajira hiyo ikitengewa wakazi wa kaunti hii.” Alisema Guru.