MFUMO UNAOTUMIKA KUSAMBAZA FEDHA ZA INUA JAMII WATAJWA KUWA DHALIMU KWA WAZEE.

Serikali imetakiwa kubadili mfumo ambao unatumika kutoa pesa za inua jamii kwa makundi lengwa ikiwemo ya wazee, walemavu na mayatima nchini.

Ni wito ambao umetolewa na wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wakiongozwa na Hassan Lodomo, ambao walisema kwamba mfumo unaotumika kwa sasa unawasababishia mahangaiko mengi wazee ambapo wanalazimika kusubiri muda mrefu kwenye foleni kabla ya kuhudumiwa licha ya umri wao.

Aidha walisema kwamba licha ya wengi wao kutumia fedha nyingi kusafiri hadi maeneo ambako wanapasa kupokea fedha hizo, mara nyingi hulazimika kurejea mikono mitupu baada ya kufeli mtandao  au hata kutopatikana majina yao.             

“Njia ambayo inatumika kuwapa pesa wazee kupitia mpango wa inua jamii unawaumiza sana. Kwa sababu licha ya umri wao wazee hawa wanalazimika kutunga foleni hadi jioni. Na hata wakati mwingine wanaaambiwa mtandao umefeli au majina yao hayapatikani hali wametumia muda mwingi sana kwenye foleni.” Alisema Lodomo.

Lodomo sasa anataka serikali kuweka mikakati itakayohakikisha fedha hizo zinawafikia wazee hao maeneo ya mashinani, ili kuwaepushia mahangaiko ya kutumia fedha nyingi kusafiri kila mara pamoja na kuwaepusha na hali ya kusubiri kwa muda mrefu kwenye foleni kabla ya kuhudumiwa.

“Ingekuwa bora na afueni sana kwa wazee hawa iwapo serikali ingebadili mfumo inaotumia kuwapa wazee fedha hizi. Pesa hizi zingetumwa maeneo ya mashinani ili kuwapunguzia wazee hawa muda na gharama ya kusafiri kuelekea maeneo wanakopokea fedha hizo kwa sababu wengi wao wanatoka mbali sana.” Alisema.