SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA SHUGHULI YA KUWAPA WAKULIMA MBUZI AINA YA GALA KUIMARISHA SHUGHULI ZA KILIMO CHA UFUGAJI.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeendeleza mikakati ya kuimarisha kilimo cha ufugaji kwa wakazi wa kaunti hiyo katika juhudi za kuimarisha mapato miongoni mwa wakazi kupitia shughuli za kilimo.

Akizungumza baada ya kuongoza shughuli ya kupeana mbuzi alfu 1,401 aina ya gala kwa makundi ya wakulima eneo la Nasukuta, gavana Simon Kachapin alisema kwamba lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kwamba hali ya uchumi wa kaunti hiyo inaimarika zaidi kupitia mifugo.

Alisema jumla ya shilingi milioni 400 zimetumika kwenye mradi huo ambao umefadhiliwa na kaunti kwa ushirikiano na benki ya dunia.

“Tumepeana mbuzi alfu 1,401 kwa makundi mbali mbali katika wadi zetu zaidi ya 11. Hii ni mbegu nzuri kwa wakulima wetu na tunataka wakulima wetu waweze kutekeleza shughuli zao za kilimo kwa njia bora ili wapate faida zaidi. Tumetumia jamla ya shilingi milioni 400 kwa mradi huu.” Alisema Kachapin.

Mshirikishi wa mradi wa Kenya climate smart agriculture Philip Ting’aa alisema aina hiyo ya mbuzi watawafaa sana wakulima hasa ikizingatiwa kaunti hiyo ni moja ya kaunti kame nchini kwani ni mbuzi ambao wanastahimili ukame.

“Mbuzi hawa watasaidia sana hasa wakati huu ambao tunazungumza kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Hasa kaunti hii ambayo ni moja ya kaunti kame, mbuzi hawa wanafaa sana kwani wanastahimili ukame.” Alisema Ting’aa.

Viongozi wa maeneo ambayo yamenufaika katika mradi huo walipongeza hatua hiyo wakisema kwamba itainua hadhi ya wakulima wa maeneo hayo kupitia aina ya mifugo wanaokuza na ambao wataweza kuimarisha mapato yao.

“Watu wetu watanufaika sana na mbuzi hawa ikizingatiwa kwamba wameimarishwa zaidi ikilinganishwa na mbuzi wetu wa kawaida. Mbuzi hawa sasa watainua hadhi ya watu wetu wanaojihusisha na maswala ya ufugaji.” Walisema.