GAVANA WA TURKANA AENDELEA KUSUTWA KWA MADAI YA KUENEZA MATAMSHI YA UCHOCHEZI.
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kumsuta gavana wa kaunti ya Turkana Jeremiah Lomurkai kwa kile wamedai kwamba ameendelea kueneza semi za chuki katika mikutano ya umma kwenye kaunti hiyo.
Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alidai kwamba katika matamshi ya hivi punde gavana huyo ameendelea kudai kwamba eneo la Lami Nyeusi katika kaunti hiyo pamoja na Silale eneo la Tiati kaunti ya Baringo yapo katika ardhi ya Turkana.
Lochakapong alisema kwamba swala la ardhi ni nyeti sana na ambalo viongozi hawapasi kutoa matamshi ya kiholela kulihusu kwani huenda hali hiyo ikaibua uhasama baina ya jamii husika, akitoa wito kwa idara za usalama kumchukulia hatua kwani imekuwa mazoea kwake kutoa matamshi kama hayo.
Aidha Lochakapong ameitaka serikali kutoendeleza ubaguzi wa kisheria ambapo baadhi ya watu wanaonekana kuwa juu ya watu wengine.
“Nilisikia gavana huyo akiendeelea kutoa matamshi ya uchochezi akiwaambia watu wa Turkana kwamba eneo la lami nyeusi liko katika kaunti ya Turkana, na pia silale kuwa iko kwenye ardhi ya Turkana. Tunataka sheria kufanya kazi kwa usawa kwa watu wote. Isiwe kwamba kuna watu wanaweza kutamaka jinsi wanavyotaka ila hawachukuliwi hatua huku wengine wakiandamwa.” Alisema Lochakapong.
Alimtaka gavana huyo kuendeleza siasa kupitia sera za kuhakikisha maendeleo kwa wananchi, badala ya kutoa matamshi ya kiholela kwa lengo la kutaka kuonekana kuwa shujaa, hali yanaweza kusababisha madhara miongoni mwa wananchi.
“Tusifanye siasa kwa kuwachochea wananchi ili kwamba tuonekana kuwa mashujaa machoni pa wananchi. Mtu afanye siasa kwa kutumia sera zitakazohakikisha miradi ya maendeleo yanaafikiwa kwa ajili ya wananchi.” Alisema.