WAKAAZI LOMUT WATAJA MIRADI YA KILIMO KUWA CHANZO CHA UTULIVU AMBAO UNASHUHUDIWA SASA.

Wakaazi wa eneo la Lomut katika kaunti ya Pokot magharibi, moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama wamesifia miradi ambayo imekuwa ikiendelezwa eneo hilo chini ya mradi wa Kenya climate smart agriculture.

Wakiongozwa na Joseph Riong’otany wakazi hao walisema kwamba tangu kuanzishwa miradi hiyo ambayo hasa inahusu kilimo na ufugaji, wengi wa vijana wameasi wizi wa mifugo na kujishughulisha na kilimo hali ambayo imeimarisha usalama.

Walisema kwamba kwa miaka mingi jamii ya Pokot imekuwa ikihusishwa na wizi wa mifugo ila sasa kupitia miradi hiyo wataweza kubadilisha dhana hiyo.

“Kwa miaka mingi jamii ya pokot imekuwa ikitazamwa kuwa inayoendeleza wizi wa mifugo. Lakini sasa miradi hii imefanya vijana wengi kujihusisha na kilimo na sasa tunalenga kubadilisha dhana hii ambayo imekuwepo kwa muda kuhusu jamii hii ya Pokot.” Alisema Riong’otany.

Aidha kina mama walisifia miradi hiyo wanayosema imewawezesha kujikimu kimaisha na kuhakikisha kwamba wanao wanahudhuria masomo, kufuatia utulivu ambao unaendelea kushuhudiwa eneo hilo linalopakana na kaunti ya Elgeyo marakwet.

“Tumekuwa na tatizo sana maeneo ya Lomut na Chesogon ambapo tumekuwa na utovu wa usalama kila mara. Ila tulipoanza kujihusisha na miradi hii kwa msaada wa Kenya climate smart, amani imedumu ambapo sasa tunapata kujikimu kimaisha na tunawapeleka watoto shule bila tatizo.” Walisema.